Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachimbaji madini waomba kuanzishwa benki yao

37830 Pic+benki Wachimbaji madini waomba kuanzishwa benki yao

Tue, 22 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (Femata), John Bina ameomba kuanzishwa kwa benki ya madini nchini itakayokuwa inatunza madini na kutunza fedha za wachimbaji.

Pia, wameomba Serikali kuweka hati ya utambulisho katika madini ya Tanzanite ili ijulikane inatokea Tanzania peke yake.

Bina akizungumza leo Jumanne Januari 22, 2019 katika mkutano wa wachimbaji, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini nchini amesema sababu ya benki hiyo itakuwa imesheheni wataalamu wa madini itaweka urahisi kwao kutunza bidhaa zao na kupata mikopo. 

“Kwa sababu katika benki hizi za kawaida kukopesheka ni kugumu sana lakini tukiwa nayo ya kwetu tutakuwa huru na wadau wote wa madini watahusika, itakuwa chini ya BoT (Benki Kuu ya Tanzania),” amesema Bina.

Pia, wamewaomba wadau na BoT kushirikiana kununua madini yaliyopo nchini ili kurekebisha na kusimamia soko la madini.

“Kwa sasa matatizo yaliyopo, wanunuzi wapo lakini hawaonekani  likitokea tatizo dogo wanaacha, Geita hali ni mbaya mno gramu moja imetoka kwenye Sh80,000 hadi Sh30,000 hivyo benki itakapokuwapo itaoongoza soko,” amesema Bina.

Amesema Tanzanite kuwekewa utambulisho utasaidia kubaini madini mengine ya aina hiyo ni bandia.

“Hata ikitangazwa katika utalii itaonekana uhalisia wake ni kutoka Tanzania na inakuwa ni nembo pekee ya kutangaza nchi,” amesema.

Pia, ameiomba Serikali kuwasemea wachimbaji wadogo wanaodaiwa katika maeneo ambayo hawakuyachimba kwa kukosa taarifa sahihi za kijiolojia.

Wachimbaji hao wameomba kuanzishwa kwa siku ya madini nchini itakayokuwa inasherehekewa Julai 5 kila mwaka pamoja na kuomba mwakilishi mmoja ndani ya Bunge.

Bina amesema wakati wachimbaji hao wanaomba leseni huangalia sehemu yenye madini lakini pindi yanapoacha kupatikana wanakimbia.

“Kinachotokea zile leseni ukienda TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) unaambiwa unadaiwa katika viwanja vyako Iringa. Tunaomba tukiyachimba mtusamehe madeni kwa sababu ni mzigo kwetu,” amesema.

Akizungumzia siku maalumu ya madini amesema kutokana na nchi kuwa na zaidi ya madini 260, amsema hakuna haja ya wao kupeleka katika maonyesho nchi nyingine.

“Tumekubaliana kuwa siku hii itaitwa Magufuli Day na tutaonyesha bidhaa zetu zote zitokanazo na madini nchini ili kuweza kuitangaza nchi kimataifa,” amesema Bina.



Chanzo: mwananchi.co.tz