Wachimbaji wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamelalamika kwa Waziri wa Madini, Anthony Mavunde bei kubwa ya nishati ya umeme migodini wanayodaiwa tofauti na matumizi yao.
Katibu wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara (Marema) Tawi la Mirerani, Rachel Njau akizungumza Septemba 26 kwenye maonyesho ya sita ya kimataifa ya teknolojia ya madini mjini Geita, amemuomba Waziri Mavunde awasaidie.
Njau amesema wachimbaji wa madini ya Tanzanite wanaodaiwa fedha na Tanesco Mirerani, wamepewa siku 14 kulipa la sivyo watakatiwa umeme.
"Tuliomba kuondolewa mita zilizopo kwani zinasoma hata kama hufanyi kazi na hata umeme ukikatika zinasoma, Waziri wetu ingilia kati suasa hili kwani wachimbaji tunateseka," amesema Njau.
Mwenyekiti wa chama cha madalali wa madini Tanzania, Jeremia Simon amesema wachimbaji wa madini ya Tanzanite wanalipa bei kubwa tofauti na wanavyotumia umeme.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema suala hilo watalifikisha kwa Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko ambaye ni Waziri wa Nishati ili kujadili hilo.
Waziri Mavunde ametoa agizo kwa ofisa wa madini wa eneo husika kufuatilia suala hilo kwa kukutana na wachimbaji hao wanaodaiwa ili kuona na wahusika hao.
Hata hivyo, Meneja wa Tanesco Mirerani, Zacharia Masatu ameeleza kuwa haiwezekani kuweka mita za luku migodini kwani unatumika mwingi.
Masatu amesema wachimbaji wanatumia umeme wa bei nafuu kuliko wanaotumia mita za Luku kwani kadiri unavyotumia umeme mwingi unalipia bei kidogo kupitia ruzuki ya serikali.
Amesema wameingia makubaliano na Kampuni ya Yono Action kwa ajili ya kukusanya madeni yao kwa wadaiwa sugu wa eneo hilo.