Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachimba mchanga kupima joto kabla uchimbaji

WACHIMBAJI.png Wachimba mchanga kupima joto kabla uchimbaji

Mon, 27 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MKUU wa Wilaya ya Kaskazini B, Rajab Ali Rajab, amewataka watumiaji wa machimbo ya shimo la mchanga lililopo Kiomba Mvua kupima joto la mwili kabla ya kuingia ili kujiepusha na maambukizo.

Akizungumza na madereva wa magari ya mchanga, wapakiaji na wasimamizi wa shimo hilo, Mkuu huyo wa wilaya alisema, kupima joto, kunawa mikono mara kwa mara, kuvaa gloves na barakoa ndio njia pekee itakayosaidia kupunguza maambukizo ya ugonjwa huo katika shughuli zao za kila siku ambazo zina mwingiliano wa watu.

Alisema serikali ya wilaya imepeleka wataalamu wa afya katika shimo hilo ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo ambao hadi sasa idadi ya maambukizo imekuwa ikiongezeka kila siku visiwani Zanzibar.

Vile vile, alisema hali ya ugonjwa huo katika wilaya yake sio nzuri kutokana na baadhi ya wananchi kukaidi agizo la serikali kuhusu katazo la mikusanyiko kwa kuhudhuria shughuli za mazishi pamoja na kushindwa kutekeleza maagizo ya wataalamu wa afya.

Alisema kuwa serikali haikatazi wananchi kuzika wapendwa wao, lakini ni vyema kwa sasa shughuli za mazishi zikatekelezwa na ndugu wa karibu na marehemu ili kuinusuru wilaya na taifa kwa ujumla dhidi ya Covid -19.

Mkuu huyo pia aliwataka wasimamizi wa shimo hilo kuzingatia makubaliano kwa kuingiza watu 200 kwa siku badala ya 600 wa awali ili kuendelea kujikinga.

Kwa upande wao wapakiaji wa mchanga wamempongeza mkuu huyo wa wilaya kwa kuwapelekea wataalamu wa afya na kuwa wanafanya shughuli zao kwa usalama wa afya zao na familia zao kwa ujumla.

Wameahidi pia kutekeleza agizo la serikali kwa kuhakikisha wanaenda katika shughuli zao kwa kuzingatia makundi waliyopangwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live