MKEMIA Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko amewataka wachenjuaji na wachimbaji wadogo wa dhahabu mkoani hapa kusajiliwa na kutambulika kisheria kama watumiaji wa kemikali ili waweze kupatiwa mafunzo yatakayowawezesha kuboresha shughuli za uchimbaji wa dhahabu na kuongeza kipato.
Dk Mafumiko aliyasema hayo mkoani Geita wakati akifungua mafunzo ya matumizi salama ya kemikali kwa wachimbaji na wachenjuaji wadogo wa madini ya dhahabu wa mkoa wa Geita yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Kanda ya Ziwa.
“Kati yenu bado kuna wadau wengi ambao wanafanya kazi za uchenjuaji na uchimbaji wa dhahabu kwa kutumia kemikali bila kusajiliwa kama Sheria inavyotaka. Pia kuna wadau wengi wanatumia baadhi ya kemikali bila kufuata taratibu za Kisheria na uingizaji wake bado haujulikani pamoja na kwamba matumizi yake kwenye uchuchenjuaji wa dhahabu bado haijazuiwa.
Kinachohitajika pekee ni wahusika kuingiza na kutumia kemikali hizo kwa kufuata taratibu ili Serikali iweze kuwa na takwimu sahihi za uingizaji na matumizi yake na kuweza kuwatambua na kuwapatia mafunzo ya matumizi salama kwa lengo la kuongeza kipato chenu na serikali kuingiza mapato kupitia shughuli za uchimbaji,” alisema.
Aidha, Mkemia Mkuu wa Serikali aliwaeleza wachimbaji na wachenjuaji wa dhahabu kwamba lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa juu ya matumizi salama ya kemikali ili kupunguza madhara na kuzingatia matakwa ya Sheria ya Kemikali na baada ya mafunzo anaamini watajisajili ili kuweza kutambulika kisheria kufanya shughuli za uchimbaji kwa kutumia kemikali.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Dhahabu Mkoa wa Geita, Christopher Kadeo akizungumzia mafunzo hayo alimshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuwapatia mafunzo ya matumizi salama ya kemikali kwa sababu yatawaongezea uelewa wa utumiaji wa kemikali kutokana na ukuaji wa teknolojia na mabadiliko makubwa katika Sekta ya madini.