Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunifu wapewa  somo kupata masoko 

89b39b147816c7d796608167045e26e5.jpeg Wabunifu wapewa  somo kupata masoko 

Thu, 20 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WABUNIFU nchini wametakiwa kutumia vizuri taarifa za mitandao kwa ajili ya kujiongezea ujuzi na kuongeza wigo wa masoko yao kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa alisema hayo wakati wa ufunguzi wa wiki ya ubunifu Tanzania ambapo kwa mkoa wa Tanga inafanyika katika kituo cha ubunifu wa kisayansi kilichopo katika kata ya Chumbageni.

Alisema kuwa nchi yetu inapitia maendeleo makubwa ya uchumi wa viwanda hivyo ni vema wabunifu wakatumika kwa ajili ya kushiriki katika harakati hizo badala ya kutumiwa vibaya na wenye nia ovu.

Alisema nchi yetu imeweza kupitia hatua mbalimbali za kujiinua kiuchumi na sasa haiwezi kukwepa kutimia teknolojia ya dijiti katika kuboresha uchumi, hivyo kuna umuhimu kubwa wa kuwa makini na taarifa ambazo mtu anatafuta kwenye mitandao na namna ya kuzisambaza ili zisilete madhara kwa wananchi na taifa.

Aidha alisema ni lazima tujifunze mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto za uchumi unaotegemea maendeleo ya teknolojia ya dijiti ili kama taifa tuweze kuona namna ambavyo tutaweza kwenda na kasi ya maendeleo hayo bila ya kuharibu tamaduni zetu na maadili yetu.

Meneja wa Kituo cha Sayansi, Gipson Kawago, alisema kuwepo kwa maonesho hayo ni fursa nzuri, hivyo ni vema kuitumia kuonesha uwezo wetu wa ubunifu.

Alisema kuwa lengo la uwepo wa maonesho hayo ni kuwasaidia wabunifu kuonesha ubunifu wao kwa jamii na kutumia kama fursa ya kujitangaza ili kujulikana ni shughuli gani wanafanya.

Meneja huyo alisema uwepo wa maonesha hayo mkoani Tanga ni fursa za kuwaibua wabunifu wachanga na wanaochipukia kuweza kujulikana na kupata fursa za kuongeza vipaji vyao.

Kawogo alisema kituo cha sayansi ni kwa ajili ya kutengeneza fursa kwa ajili ya watoto na vijana kuweza kufanya majaribio ya kisayansi, teknolojia na mahesabu kwa vitendo zaidi.

"Katika mashule yetu walimu wanajitahidi kufundisha zaidi masomo ya sayansi kwa kujenga maabara lakini sio wanafunzi wote wanaweza kupata fursa ya kushiriki kwenye mazoezi hayo hivyo kituo hicho kipo kwa ajili ya kutoa fursa hiyo”alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz