Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge wataka mifumo ya Tehama Bandari Dar iboreshwe

5c4fbe26847676e3fcd84155019edda4 Wabunge wataka mifumo ya Tehama Bandari Dar iboreshwe

Wed, 16 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bunge limeshauri serikali iboreshe mifumo ya Tehama inayotumiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania kuwezesha ufanisi wa huduma za bandari, hatua itakayoongeza imani ya watumiaji.

Aidha, mhimili huo wa kutunga sheria umeshauri serikali kuona umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi katika uendeshaji wa reli.

Ushauri huo umo kwenye taarifa ya mwaka ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa kipindi cha Januari 2021 hadi Februari 2022, iliyojadiliwa, ikaungwa na wabunge jana bungeni.

Bunge kupitia taarifa hiyo iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati, Moshi Kakoso lilisema ulinzi wa mizigo inayopokewa katika Bandari ya Dar es Salaam uimarishwe kwa kutumia Tehama na mbinu nyingine za kiusalama.

"Kwa kuwa changamoto hizo zinachangia wateja wakubwa wa bandari kutotumia bandari hizo, hivyo basi Bunge linashauri mifumo ya Tehama inayotumiwa na mamlaka ya bandari iboreshwe," alisema Kakoso.

Kuhusu umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi katika uendeshaji wa reli, ilielezwa kwamba upungufu wa vichwa 45 pamoja na mabehewa, imekuwa ni changamoto inayoathiri ufanisi na mchango wa sekta kwenye maendeleo ya ustawi wa uchumi.

"Kwa hiyo basi serikali ione umuhimu wa kuishirikisha sekta binafsi katika uendeshaji wa reli," ilisema taarifa hiyo iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati, Moshi Kakoso.

Bunge limeshauri pia serikali iangalie uwezekano wa kupata mkopo wa masharti nafuu utakaowezesha ununuzi wa vichwa hivyo 45 ili kuboresha huduma ya usafiri wa reli na usafirishaji, hatimaye kuongeza mchango wa sekta ya reli kwenye maendeleo ya taifa.

Aidha, Bunge limeshauri ujenzi wa reli unapofanyika, tahadhari kubwa ichukuliwe kuepusha uharibifu wa miundombinu kama ilivyobainika uharibifu uliotokana na mabadiliko ya tabianchi hususani katika maeneo ya Godegode na Mto Mkondoa kutokana na mafuriko.

Bunge limetaka pia serikali kuisimamia Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kukutana na wadau na watoa huduma kuona chanzo cha kupungua kwa miamala ya simu kwa lengo la kutatua changamoto hizo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live