Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeshauri magari ya serikali yawe na mfumo wa kutumia gesi asilia ili kupunguza gharama. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Daniel Sillo alisema hayo bungeni, Dodoma wakati akiwasilisha taarifa kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2021.
Taarifa hiyo pia inahusu tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2021/2022, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2022/2023 na mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/2023. Sillo alisema nchi nyingi hivi sasa zinahama katika matumizi ya nishati zinazozalisha hewa ukaa na kwenda katika nishati jadidifu. “Kuna baadhi ya rasilimali tusipozitumia hivi sasa baadaye zinaweza zisiwe na thamani yakiwamo makaa ya mawe,” alisema.
Alisema inapaswa kuhakikisha rasilimali zinavunwa kwa uangalifu na kwa maslahi mapana ya taifa. “Kamati inashauri magari ya serikali yawe na mfumo wa kutumia gesi asilia kama ilivyo kwa malori ya kampuni ya Dangote. Hatua hii sio tu kwamba itapunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje, vilevile itapunguza nakisi ya urari wa jumla wa malipo na biashara,” alisema.
Alisema pia kamati hiyo inaishauri serikali kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ili walau yawe na uwezo wa kugharamia miradi ya maendeleo angalau kwa asilimia 40. Alisema katika mwaka wa fedha 2022/2023 serikali imepanga kutumia Sh trilioni 41.06 sawa na ongezeko la asilimia 8.1, ikilinganishwa na Sh trilioni 37.99 mwaka 2021/2022 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. “Takwimu zinaonesha mapato ya ndani yanazidi matumizi ya kawaida kwa kiasi cha Sh trilioni 3.03.
Hii maana yake ni kwamba mapato yote ya ndani yanaweza kugharamia matumizi ya kawaida peke yake na asilimia 8.3 tu ya miradi yote ya maendeleo,” alisema. Kamati hiyo pia imeishauri serikali ipunguze kukopa kwenye soko la ndani ili kuwe na mikopo kwenye sekta binafsi na badala yake iangalie nyanzo vya mikopo ya nje yenye masharti nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Sillo alisema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 serikali imepanga kukopa katika soko la ndani Sh trilioni 2.05 sawa na ongezeko la asilimia 11.72 ikilinganishwa na Sh trilioni 1.84 mwaka 2021/2022. Kamati hiyo imeishauri serikali iendelee kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili iondokane na utegemezi wa kibajeti kwa kuwa uchumi wa nchi wahisani umetetereka kutokana na janga la Covid-19 na vita ya Urusi na Ukraine.