Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge washauri mambo 5 uchumi

BUNGE WER Wabunge washauri mambo 5 uchumi

Tue, 20 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeishauri serikali ifanye mambo matano ili kunusuru uchumi ikiwemo deni la serikali lisiathiri uchumi huo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Daniel Sillo alitoa ushauri huo bungeni Dodoma jana wakati anawasilisha taarifa ya kamati hiyo kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2022.

Taarifa aliyoisoma Sillo pia ilihusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2023/24, tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2022/23 na mapendekezo ya serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

Alisema uchambuzi wa kamati hiyo ulibaini kwamba hadi Aprili mwaka huu, deni la serikali lilikuwa ni Sh trilioni 79.1 ukilinganisha na deni la Sh trilioni 69.26 katika kipindi kama hicho mwaka jana sawa na ongezeko la asilimia 13.9 (Sh trilioni 9.84).

Sillo alisema ongezeko la deni limetokana na sababu mbalimbali ukiwamo ukopaji kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, kutolewa kwa hatifungani maalumu yenye thamani ya Sh trilioni 2.18 kwa ajili ya kulipa deni la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) linalohusu michango ya watumishi waliokuwa kwenye utumishi kabla ya mwaka 1999 na malimbikizo ya riba ya deni la nje.

Alisema ingawa deni la serikali ni himilivu kwa viwango vyote vya kimataifa, kamati hiyo inaendelea kuishauri serikali iendelee kuangalia uwezekano wa kujipima uhimilivu wa deni kwa kutumia kiashiria cha makusanyo ya mapato ya ndani kwa ulipaji wa deni.

Alisema kwa kuwa serikali ilitoa hatifungani maalumu yenye thamani ya Sh trilioni 2.18 kwa ajili ya kulipa deni la PSSSF kamati inashauri serikali ifanye mapitio ya viwango vya pensheni ya wastaafu kabla ya miaka ya 1990 ili viendane na hali halisi ya sasa.

Pia kamati hiyo imeishauri serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Wizara ya Fedha na Mipango iweke mikakati ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kukabili mfumuko wa bei unaotokana na uagizaji wa bidhaa ili kutokuathiri uchumi wa taifa.

“Kamati inaendelea kuishauri serikali kuendelea kutumia nyenzo mbalimbali za sera ya fedha ili riba za mikopo ziwiane na kiwango cha mfumuko wa bei wa asilimia 4.3. Kuwe na utaratibu maalumu utakaowezesha watumishi wa umma kupata mikopo yenye riba nafuu,” alisema.

Sillo alisema kwa kuwa soko la bidhaa Tanzania limefanya mauzo ya bidhaa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2018 hadi 2022 ambapo tani milioni 107.06 za bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 12,223.26 zimeuzwa kamati inaishauri serikali iongeze idadi ya mazao na bidhaa zitakazokuwa zinauzwa katika soko hilo na kuongeza idadi ya wanunuzi wanaoshiriki katika kununua bidhaa katika soko hilo.

Wakati huohuo, kamati hiyo imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza Mwongozo wa Ushirikiano na Washirika wa Maendeleo. Kamati hiyo pia imempongeza Rais Samia kwa kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa kimataifa na kwamba jitahada zake zimeiwezesha nchi kufikia ufanisi wa asilimia 99.14 katika kupokea fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Alisema katika mwaka wa fedha 2022/23 serikali ilitarajia kupata Sh trilioni 4.65 kutoka kwa washirika wa maendeleo na hadi Aprili mwaka huu ilikuwa imepokea Sh trilioni 4.61 sawa na asilimia 99.14. “Kati ya fedha hizo shilingi trilioni 1.50 ni misaada na mikopo nafuu ya kibajeti; shilingi bilioni 85.4 ni misaada na mikopo nafuu ya mifuko ya pamoja ya kisekta; na shilingi trilioni 2.22 ni misaada na mikopo nafuu ya miradi ya maendeleo,” alisema.

Serikali pia imeshauriwa ichochee mauzo ya dhahabu na makaa ya mawe nje ya nchi na idhibiti uagizwaji wa bidhaa zisizo za msingi ili kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live