Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge wapigilia msumari agizo la Samia TBA

TBA MAJENGO.jpeg Wabunge wapigilia msumari agizo la Samia TBA

Thu, 8 Sep 2022 Chanzo: Habarileo

Wabunge wameshauri Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza uwezo wa kujenga nyumba nyingi zitakazosaidia kupunguza uhaba kwa watumishi wa umma badala ya kuendelea kutegemea ruzuku ya serikali.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Jerry Silaa, alitoa ushauri jana jijini hapa baada ya kufanya ziara ya kukagua ujenzi wa miradi mbalimbali unaotekelezwa na TBA.

Kamati hiyo ilitembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa makao makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ujenzi wa nyumba 20 za viongozi kisasa pamoja na mradi wa ujenzi wa nyumba 150 za watumishi eneo la Nzuguni.

Alisema ni vyema wakala huyo akapanua wigo wa kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa majukumu yake badala ya kutegemea ruzuku ya serikali pekee.

“Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan, alishauri wakala huo kutafuta namna ya kuanza kufanya biashara ili kukidhi mahitaji makubwa ya nyumba kwa watumishi yaliyopo hivi sasa.

“Agosti 31, mwaka huu kamati yetu ilikutana na TBA na leo hii tulikubaliana kuja kutembelea miradi ambayo wanaitekeleza na kamati imeridhishwa na utekelezaji wa miradi yote.

“Kama ambavyo Rais alitoa ushauri kwa TBA pia sisi Bunge tunaishauri TBA kuona namna ambavyo inaweza kufanya kazi kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza uwezo wake wa kujenga nyumba kwa wingi ili kukabili uhaba uliopo hivi sasa badala ya kuendelea kutegemea ruzuku kutoka serikalini.”

Pia amesisitiza Wakala huyo kuhakikisha wanaitumia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa kuingia mikataba na sekta binafsi ili kupata tija inayokusudia.

Silaa alisema kamati hiyo inashauri taasisi nyingine zenye dhamana ya barabara, maji na umeme kupeleka miundombinu katika maeneo ambayo miradi hiyo inatekelezwa.

Mtendaji Mkuu wa TBA, Daudi Kondoro alisema ameshaanza makubaliano na baadhi ya sekta binafsi kujenga jengo kubwa eneo la Magomeni Dar es Salaam na nyumba ya makazi ya ghorofa moja eneo la Mikocheni.

Alisema katika ujenzi wa makao makuu ya Shirika la Umeme (Tanesco), wameshiriki katika ujenzi na ubunifu walifanya watu wengine. Vilevile ujenzi wa nyumba kwa ajili ya watumishi Nzunguni jijini Dodoma, wamepanga kujenga nyumba 3,500 lakini wameanza na nyumba 150 ambazo zitakamilika Desemba mwaka huu.

“Mwezi Oktoba mwaka huu tunapanga kuwa tumekamilisha nyumba 50, Novemba pia 50 na zingine 50 za mwisho tunapanga kuzikamilisha ifikapo Desemba mwaka huu,” alisema.

Hata hivyo, alisema hadi sasa katika ofisi yao ya mkoa wameshapokea maombi ya watumishi 900, ambao wanahitaji nyumba kwa ajili ya makazi.

Chanzo: Habarileo