Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge wakataa  madalali soko la Ndugai

025e9646052665423703449467d212bc.jpeg Wabunge wakataa  madalali soko la Ndugai

Thu, 20 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WABUNGE wameishauri serikali idhibiti madalali katika kupata vizimba na ushushaji wa mizigo katika soko la kisasa la Ndugai jijini Dodoma.

Pia wameshauri mpango wa kuhamisha wafanyabiashara wa soko la Sabasaba kwenda soko la Ndugai usitekelezwe.

Wabunge walitoa ushauri huo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ilipotembelea soko hilo kuona hali ya utoaji huduma. Serikali imetumia Sh bilioni 14.6 kujenga soko hilo.

Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe (CCM) alisema kutoimarika kwa biashara kwenye soko hilo kunasababishwa na madalali kuhodhi vizimba na kuzuia magari yasishushe mizigo.

"Madalali ni kikwazo kikubwa pale, unaweza kuta wamelipia vizimba wakisubiri biashara ichanganye, hata yale malori tuliyokuta wakishusha mizigo tumeyakuta pale kwa sababu Kamati ya Bunge imetembelea ndio maana baada ya muda hakuna hata mkungu mmoja wa ndizi, imeenda wapi?" alihoji.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema wamebaini changamoto ya madalali na wameamua kutoa siku 14 kwa wote waliolipia vizimba kuanzisha biashara la sivyo watanyang’anywa.

Hata hivyo, Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu (CCM) alipinga wazo la kutaka kuhamishwa soko la Sabasaba.

"Hatupaswi kuwaondoa wafanyabiashara wa soko hilo, liache lifanye kazi na tuje na mfumo mzuri wa kuhakikisha miradi kama hii iliyotumia fedha nyingi inakuwa na ufanisi. Kama mnataka kuwahamisha basi tuwatoe wale waliozidi na wanaopanga biashara chini ndio waende soko la Ndugai," alisema.

Mbunge wa Viti Maalumu, Angelina Malembeka (CCM) alisema wazo la uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutaka kuwahamishia wauza mbao na gereji katikati ya jiji kwenye soko la Ndugai kwa lengo la kuhamasisha biashara si sahihi.

Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana (CCM) alisema soko la Ndugai limejengwa eneo mwafaka hasa kwa kuwa viwanja vingi vimetengwa maeneo ya karibu ya Mtumba, Nzuguni na Chamwino hivyo wanatarajia baada ya watu kujenga watakuwa wakilitumia.

Mbunge wa Ulyankulu, Rehema Migilla (CCM) alishauri uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ukitumie chombo kilicho chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuufanyia tathmini mradi wa soko la Ndugai.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Abdallah Chaurembo alishauri zifanyike tafiti kabla ya kutekeleza miradi katika halmashauri ili iwe na tija.

"Ni vyema utafiti wa kina ufanyike ili kuepuka kuweka fedha za umma kwenye miradi ambayo haina matokeo, tuna soko la Machinga Complex limetumia fedha nyingi na hakuna kitu, kule Temeke kuna soko limejengwa halifanyi vizuri na pia wanataka kujenga jingine, hili lifike mwisho," alisema Chaurembo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu alisema watafanya mapitio ya mpango wa biashara wa soko la Ndungai ili uendane na kile kilichokusudiwa.

"Mradi wa soko la Ndugai ulibuniwa kwa kuangalia long time plan (mpango wa muda mrefu) kwa kuwa Dodoma imekuwa ni makao makuu ya nchi, lakini pia ongezeko la watu, hivyo ni kweli zimewekwa Sh bilioni 14.6, lakini ukiangalia makisio ya marejesho kiasi hicho cha fedha kitarudi.”

"Soko si gereji, soko sio kuuza mbao, soko lile linatakiwa kuwa la kimataifa ambalo litavutia watu kwenda kununua mahitaji yao kwa kuwa bidhaa ndio zinazosababisha watu kwenda kufuata huduma," alisema Ummy.

Meneja wa soko la Ndugai, Steve Maufi alisema hadi sasa vizimba 318 kati ya 366 vimepata wateja, maduka 161 kati ya 175 pia yamechukukiwa na bucha saba kati ya tisa zimepata wapangaji na mgahawa mmoja umepata mpangaji na mmoja bado haujapata.

Alisema ili kuwavutia wafanyabiashara, uongozi umepunguza gharama za upangishaji kutoka Sh 90,000 hadi Sh 30,000 kwa eneo lenye mita za mraba 7.8 na pia kutoka Sh 70,000 hadi Sh 20,000 kwa eneo la mita za mraba 5.8.

Chanzo: www.habarileo.co.tz