Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge waibana BoT kupanda kwa bei ya bidhaa

16436 PIC+BOT TanzaniaWeb

Sun, 9 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Wakati Serikali ikisema kuwa mfumuko wa bei umepungua, baadhi ya wabunge wamehoji kwa nini bei za bidhaa muhimu zinapanda kila siku.

Wabunge waliyasema hayo jana wakati wakichangia katika semina iliyoendeshwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), juu ya majukumu ya benki hiyo. Semina hiyo ilifanyika mjini Dodoma.

Mbunge wa Mafinga Mjini (CCM), Cosato Chumi alisema taarifa za BoT zinaonyesha kuwa wamedhibiti mfumuko wa bei katika bidhaa muhimu, lakini mtu akienda sokoni uhalisia wa bei unaonyesha zinapanda kila kukicha.

Alisema anahusisha kupanda kwa bei kwa bidhaa muhimu na kule kwa bei ya mafuta akitoa mfano kuwa hata kama bei ya chakula iko chini kuna gharama za usafirishaji zinazohusisha vyombo vya moto na mafuta.

“Ningependa nielimishwe hizi ni theory (nadharia) tu kuwa mfumuko wa bei umedhibitiwa ama ziko katika uhalisia kwa sababu katika uhalisia mimi na wananchi wangu wa kule Mafinga hatuoni chochote,” alisema Chumi.

Mbunge wa Hanang (CCM), Dk Mary Nagu alisema kuna njia mbili za kupunguza mfumuko wa bei akizitaja kuwa ni ile inayopandisha uchumi na inayouathiri.

Alisema namna bora ya kudhibiti mfumuko wa bei ni kuongeza uzalishaji ili bidhaa ziwe nyingi kuliko fedha.

“Je hili linafanyika na kama linafanyika ni kwa kiasi gani,” alihoji.

Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftaha Nachuma alihoji kwa nini mzunguko wa fedha mtaani hivi sasa ni mdogo ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita.

Kuhusu Benki ya FMBE iliyofilisiwa na BoT, mbunge wa Jang’ombe (CCM), Ally Omary alisema wateja wengi wa benki hiyo upande wa Zanzibar waliweka fedha zao baada ya kupata kiinua mgongo, lakini hadi leo hatima yao haijulikani.

“Tunataka kujua hatima ya hawa walioweka fedha zao benki nini?” alihoji Ally na kuungwa mkono na Asha Abdallah Juma (viti maalum-CCM).

Akijibu hoja hizo, naibu gavana wa BoT, Yamungu Kayandabila alisema majibu watayatoa kwa njia ya maandishi kwa wabunge.

Pia alisema Serikali imechukua hatua dhidi ya wizi wa kutumia mitandao kwenye benki akizitaja kuwa ni pamoja na kuimarisha mifumo mara kwa mara na kuwa na mifumo bora na ya kisasa ya teknolojia habari na mawasiliano.

Chanzo: mwananchi.co.tz