Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge EALA wataja kero bandarini licha ya ufanisi kuongezeka

Wabunge Ealaaa.png Wabunge EALA wataja kero bandarini licha ya ufanisi kuongezeka

Thu, 8 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wameonyesha changamoto mbili zinazowaathiri watumiaji wa huduma za bandari na ushoroba wa kati, wakihoji hatua zinazochukuliwa na mamlaka kukabiliana na hilo.

Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji (CTI-EALA) wa Bunge hilo wakiongozwa na mwenyekiti wao, Rutazana Francine wameonyesha changamoto ya ucheleweshwaji wa mizigo unaosababisha ongezeko la gharama na rushwa kwa wafanyabiashara, na ufinyu wa sehemu za kuhifadhi mizigo.

Wabunge hao wameyaeleza hayo walipofanya ziara katika bandari ya Dar es Salaam leo Februari 8, 2024.

“Tulikuja hapa tangu Februari 4, 2024 kukutana na wadau kuanzia waendeshaji, wawekezaji, wafanyabiashara na maofisa forodha wa hapa na nchi wanachama. Tumejadili namna kazi za bandari zinavyochangia ufanisi wa shughuli zao na licha kuwa tumeridhishwa na utendaji bado kuna changamoto chache zilizotajwa na wadau,” amesema Rutazana ambaye pia ni mwakilishi kutoka Rwanda.

Mwenyekiti huyo amehoji kama mamlaka imeahidi mizigo yote inatakiwa iondoke bandarini kwa siku zisizozidi tano, inakuwaje bado kuna malalamiko ya mizigo kuchelewa na wafanyabiashara wanatozwa faini kwa hilo?

“Tumekuja kupata elimu na tumekutana na wanaolalamika kucheleweshewa mizigo…Suala jingine ni kuongezeka kwa nahitaji ya bandari je, kuna maeneo mengine ya kuhifadhi mizigo ili kuongeza ufanisi?” amehoji Rutazana.

Akijibu hilo, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mussa Biboze amesema: “bandari inafanya kazi kwa ufanisi na tunahakikisha baada ya mizigo yote kushushwa inakamilisha shughuli zote za kiforodha kuanzia saa mbili hadi siku tano.”

“Ni kweli zipo changamoto ila ni chache sana na mara nyingi ni kwa maofisa usafirishaji au kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya documents (hati na vibali) hata hivyo haya yanafanyiwa kazi kwa haraka,” ameongeza.

Kwenye ufinyu wa maeneo, Biboze amesema mamlaka imeanza matumizi ya bandari kavu ya Kwala ambayo ni kubwa zaidi na inatarajiwa kupunguza msongamano wa mizigo kwa hadi asilimia 60.

“Tuna bandari kavu ya Kwala ambayo imeanza kufanya kazi, pia kilomita kadhaa kutoka hapa tuna eneo jingine la Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) licha ya kwamba ni dogo, nalo tuna mpango wa kuanza kulitumia kwa baadhi ya huduma,” amesema.

Mjumbe mwingine wa CTI – EALA, David Ole Sankok ameonyesha kuridhishwa na utendaji waliuona na kusema Tanzania bado ina maeneo zaidi ya kuwekeza kwenye uchumi wa buluu kutokana na kuzungukwa na vyanzo vingi maji, lakini alitoa changamoto kwa nchi za ukanda huu kuongeza uwekezaji ili usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi uwe mkubwa kuliko uingizaji.

“Maendeleo yanapatikana kama tutasafirisha zaidi bidhaa nje tumeona hata hapa tuna miundombinu ya kutosha ya kufanya hivyo, ila bidhaa za kusafirisha zipo wapi? Sasa tumeanza na bidhaa za ngozi,” amesema Ole Sankok.

Ameongeza kuwa ziara kama hizo zinasaidia wao kuona hali halisi ya maeneo na miundombinu ya biashara na uwekezaji ili waweze kuja na sera na sheria zitakazo saidia nchi za ukanda huo kuongeza ufanisi, ili kufikia malengo ya kuongeza usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live