Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeiingiza Zanzibar kwenye mpango mkakati wa miaka mitano 2022/27 unaolenga kuchangia ukuaji shirikishi wa uchumi. Mpango huo unaolenga kukuza uchumi ambao ni shirikishi ulikuwa unatekelezwa Tanzania Bara pekee, lakini baada ya shirika hilo kufungua ofisi visiwani humo, Zanzibar nayo imejumuishwa. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hamza Hassan Juma alisema uwepo wa WFP utasaidia kuimarisha ushirikiano wa kimkakati uliodumu kwa miongo sita sasa.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeiingiza Zanzibar kwenye mpango mkakati wa miaka mitano 2022/27 unaolenga kuchangia ukuaji shirikishi wa uchumi. Mpango huo unaolenga kukuza uchumi ambao ni shirikishi ulikuwa unatekelezwa Tanzania Bara pekee, lakini baada ya shirika hilo kufungua ofisi visiwani humo, Zanzibar nayo imejumuishwa. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hamza Hassan Juma alisema uwepo wa WFP utasaidia kuimarisha ushirikiano wa kimkakati uliodumu kwa miongo sita sasa. “Uwepo wa WFP ni kielelezo cha dhamira yao kusaidia mipango ya maendeleo ya muda mrefu ya Zanzibar. Tunaishukuru WFP sasa ipo Zanzibar,” alisema Juma. Mkurugenzi Mwakilishi wa WFP nchini, Sarah Gordon alisema wamejitolea kuunga mkono wananchi wa Zanzibar katika kufanikisha dira ya maendeleo ya kisiwa hicho ya 2050 na malengo endelevu. Mbali na hilo, WFP ilikabidhi ndege zisizo na rubani kwa Tume ya Kusimamia Maafa ili kufuatilia hatari katika maeneo yanayokumbwa na majanga. “WFP tutatoa mafunzo kwa tume kwa ajili ya kutoa elimu na ujuzi ili kuwa na marubani walioidhinishwa kuzirusha ndege hizi,” alisema Gordon.