Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeonya kuwa, upatikanaji wa ngano ya bei nafuu katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki kuna uwezekano mkubwa ukaathiriwa na mienendo ya biashara ya kimataifa.
WFP imesema hayo katika taarifa yake ya hivi karibuni kuhusu athari za kusitishwa Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi kwa nchi za mashariki mwa bara la Afrika na kusema kuwa, uzalishaji wa ngano wa ndani ya nchi za Afrika umeendelea kuwa wa kiwango cha chini ya mahitaji ya matumizi katika nchi nyingi za ukanda wa mashariki mwa Afrika.
Katika taarifa yake hiyo, WFP imetahadharisha kwa kusema: "Kuna uwezekano mkubwa upatikanaji wa ngano ya bei nafuu kwa nchi za mashariki mwa Afrika ukaathiriwa na mienendo ya biashara ya kimataifa, kwa kuzingatia utegemezi mkubwa wa bidhaa za nafaka kutoka Bahari Nyeusi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya ngano ya ndani na sarafu dhaifu za ndani nchi za Djibouti, Somalia na Sudan.” Meli ya nafaka kutoka Ukraine kwa ajili ya nchi za mashariki mwa Afrika
Takwimu za WFP zinaonesha kuwa matumizi ya ngano ni ya asilimia 67 na asilimia 38 ya jumla ya matumizi ya nafaka nchini Djibouti na Sudan kwa utaratibu huku kwa upande wa nchi za Ethiopia, Kenya na Somalia matumizi ya ngano yakiwa ni chini ya asilimia 24 ya jumla ya matumizi ya nafaka.
Djibouti na Somalia zinategemea tu uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao ya ndani ya ngano.
Shirika la WFP aidha limesema: “Sehemu kubwa ya mahitaji ya ngano nchini Kenya na Sudan inakidhiwa na uagizaji wa bidhaa kutoka nje. Ethiopia ndiyo pekee iliyo na kiwango cha chini cha kuagizia nafaka kutoka nje kwani uzalishaji wa ndani wa mwaka jana 2022 ulikidhi asilimia 82 ya mahitaji yote ya matumizi ya ndani ya ngano.”