Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

WB yazuia msaada wa Sh112 bilioni kwa Tanzania

20585 PIC+WB TanzaniaWeb

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Benki ya Dunia imezuia msaada wa zaidi ya Sh112 bilioni kwa Tanzania ikipinga marekebisho ya Sheria ya Takwimu ya Septemba 2018 ikisema yanaweka masharti yanayodhibiti uhuru wa kujieleza.

Fedha hizo zilikuwa ni kwa ajili ya kusaidia shughuli za takwimu zinazofanywa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS).

Alipoulizwa na Mwananchi kwa njia ya simu kuhusu barua hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dotto James alisema hakuna msaada ambao Serikali imeomba.

“Serikali haijawahi kuomba wala kuwa kwenye mchakato wa kukopa dola 50 milioni (za Kimarekani) kwenda kwenye kazi za Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Mimi kama Katibu Mkuu nasema hatujawahi kuandika barua kuomba hizo fedha,” alisema James.

Huku akimtaka mwandishi azungumze na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Dotto alisisitiza kutokuwepo kwa maombi ya fedha hizo.

Hata hivyo, taarifa hiyo yas Benki ya Dunia kwenda kwa mtandao wa Freedom.com haizungumzii mkopo, bali fedha ambazo taasisi hiyo ya kifedha imezitenga kwa ajili ya kufadhili miradi tofauti, na hasa ya ukusanyaji taarifa za kitakwimu, kama sensa ya watu na makazi.

Awali ofisa habari wa taasisi hiyo nchini, Loy Nabeta alithibitisha taarifa hiyo kwa baruapepe, akisema ilitolewa kujibu swali la mtandao wa Freedom.org.

“Ni kweli. Taarifa ni ya kweli, ni taarifa iliyotolewa na Benki ya Dunia ikijibu swali kutoka kwa Freedom.org,” alisema Nabeta.

Alipotafutwa baadaye kwa njia ya simu, Nabeta alisema baada ya tamko hilo, benki hiyo haitaongeza neno lolote.

Hivi karibuni, Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015 (Miscellaneous Amendments (No.3) Bill 2018).

Taarifa iliyopatikana katika mtandao wa Eye on Global Transparency jana imesema Benki ya Dunia imesikitishwa na masharti yaliyowsekwa katika uhuru wa kujieleza.

“Benki ya Dunia ‘imesikitishwa’ na mwendelezo wa vikwazo dhidi ya uhuru wa kujieleza katika takwimu nchini Tanzania,” tovuti ya eyeonglobaltransparency.net inaikariri taarifa hiyo ya Benki ya Dunia Tanzania.

Sababu ya WB kuzuia msaada

Taarifa hiyo imesema Benki ya Dunia inayaona marekebisho hayo yanakwenda kinyume na viwango vya kimataifa kama vile Kanuni za Msingi za Takwimu za Umoja wa Mataifa na Mkataba wa Afrika wa Takwimu.

Tovuti hiyo imesema kuwa Benki ya Dunia imewasilisha maoni yake kwa mamlaka husika, ikisema kuwa iwapo marekebisho hayo yatapitishwa yatakuwa na athari katika utafutaji na matumizi ya takwimu rasmi na zisizo rasmi, vitu ambavyo ni msingi muhimu kwa maendeleo ya nchi, tovuti hiyo imekariri taarifa ya Benki ya Dunia.

Mtandao wa Eyeonglobaltransparency.net pia umekariri taarifa ya Benki ya Dunia ikieleza kuwa haioni kama huu ni muda muafaka kuendelea na mazungumzo ya kuunga mkono ujenzi wa mfumo endelevu wa takwimu.

Misaada ya WB kwa takwimu

Mtandao huo umesema msaada huo ulilenga kusaidia kazi za Takwimu ikiwa pamoja na kuijengea uwezo Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na kusaidia bajeti yake kwa miaka kadhaa.

Benki ya Dunia imekuwa ikisaidia kazi za takwimu kwa nchi mbalimbali duniani, huku Tanzania ikishirikiana kitakwimu na benki hiyo, japo haziwekwi wazi.

Mbali na msaada huo, tovuti ya benki hiyo inaonyesha miradi mingine miwili ya Takwimu kwa Tanzania ya Dola 10 milioni na Dola 8 milioni, lakini yote ikiwa na malengo yanayofanana ya ukusanyaji wa taarifa, iliyobuniwa mwaka 2017, lakini bado haijaanza kazi.

Maoni ya wadau

Baadhi ya wadau wa Sheria na Uchumi wameyazungumzia marekebisho ya Sheria ya Takwimu na matokeo ya hatua ya Benki ya Dunia wakiitaka Serikali kuwa sikivu.

Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatma Karume amesema marekebisho hayo yameifanya Sheria ya Takwimu kuwa mbaya.

“Hiyo sheria imetungwa na Serikali na kupelekwa bungeni, wabunge wakaipitisha, ni sheria mbaya,” alisema Karume.

Aliongeza: “Ni mbaya kwa sababu inaifanya Serikali kuwa msahafu na kwamba sheria na takwimu zozote zitakazotolewa na Serikali ni msahafu.”

Alidai kuwa Serikali haina nia njema na huenda kuna kitu inakificha nyuma ya sheria hiyo.

“Maana yake sasa Serikali itakuwa inatoa takwimu zisizopingwa. Kwa nini sheria na takwimu ziwe neno la Mungu? Kama Serikali inaamini katika ukweli na uwazi kwa nini haitaki kukosolewa? Utaikosoaje Serikali bila kuwa na takwimu mbadala? Yaani mtu akija na takwimu mbadala ndiyo atiwe ndani? Hiyo haikubaliki,” alisema Karume.

Mbali na Sheria, Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi alisema Serikali isipoisikiliza Benki ya Dunia itaukosa msaada huo.

“Itategemea, kama Serikali itasikiliza Benki ya Dunia na kufanya marekebisho, basi itaupata huo msaada, lakini isiporekebisha itazikosa fedha. Tusubiri tuone kama watasikiliza,” alisema Profesa Ngowi.

Hivi karibuni mkurugenzi wa taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze aliikosoa sheria hiyo katika makala yake iliyochapishwa katika gazeti la The East African, Septemba 21.

Eyakuze amegusia marekebisho ya kifungu cha 24A(2) katika makala hiyo kinachosema:

“Mtu hatasambaza au vinginevyo kuwasilisha kwa umma taarifa yoyote ya takwimu inayolenga kupinga, kupotosha, au kushusha takwimu rasmi,” aliandika Eyakuze katika makala yake.

“Kifungu hiki kinamaanisha kuwa kama takwimu rasmi haziko sahihi (au hata zinazozua mjadala), kwa hiyo kuonyesha hilo tatizo au kusahihisha itakuwa ni kinyume cha sheria.

“Maoni yoyote yanayohoji au yanayokosoa takwimu rasmi yatahesabika kuwa kinyume cha sheria chini ya marekebisho mapya ya sheria, bila kujali kama maoni hayo yako sahihi au vipi.”

Amefafanua kuwa kifungu hicho kinakataza kuhakiki taarifa ikimaanisha taarifa zote ziko sahihi.

“Kwa hiyo kuchapisha takwimu zozote zinazochanganya, au zinazoleta utata kwa takwimu rasmi kutakuwa kumekatazwa kwa marekebisho hayo,” alisema Eyakuze.

Mbali na Eyakuze, taasisi ya Twaweza nayo imehoji mipaka ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika kuweka viwango vya ukusanyaji wa takwimu kwa ujumla.

“Kifungu cha 17(3)(c) kinaitaka NBS kuweka viwango vya ukusanyaji, uchambuzi na uchapishaji wa takwimu kuhakikisha usawa na ubora, usahihi wa taarifa na upatikanaji wake.”

Chanzo: mwananchi.co.tz