Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyanzo vipya vya mtaji viongezwe kufanikisha ujenzi wa viwanda nchini

22115 Pic+viwanda TanzaniaWeb

Sun, 14 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Suala la mtaji kwa ajili ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda bado ni changamoto licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali pamoja na sekta binafsi kujenga uchumi wa viwanda.

Mpaka mwishoni mwa mwaka 2016, taarifa za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kulikuwa na Watanzania milioni 2.599 walioajiriwa kwenye sekta rasmi ambao waliongezeka kutoka milioni 2.334 waliokuwapo mwaka 2015.

Kama ilivyo kwenye viwanda ambako inapewa nafasi kubwa kufanikisha sera ya ujenzi wa uchumi imara, sekta binafsi ndio inayoajiri watu wengi zaidi.

Ripoti hiyo ya NBS ijulikanayo kama 2016 Employment and Earnings Survey (EES) inaonyesha kati ya ajira zilizokuwapo, zaidi ya milioni 1,748 zilitolewa na sekta binafsi huku Serikali ikiajiri watu 850,616 pekee.

Wengi wa watumishi hao (asilimia 22.9), ripoti inasema walikuwa wanalipwa kati ya Sh500,001 na Sh900,000 kwa mwezi huku sekta binafsi ikiwa na watu wengi zaidi (asilimia 17.8) wanaolipwa kati ya Sh150,001 hadi Sh300,000 na wengine, asilimia 14.6 wakilipwa kati ya Sh100,001 mpaka Sh150,000.

Asilimia 4.5 ya watumishi waliokuwapo mwaka 2016, ripoti inasema walikuwa wanalipwa zaidi ya Sh1.5 milioni kwa mwezi.

Uchumi wa viwanda, pamoja na mambo mengine unakusudiwa kutatua changamoto kuu mbili ambazo ni kutoa ajira zaidi na kuongeza uzalishaji wa huduma za bidhaa kukidhi soko la ndani.

Sekta hiyo inatarajiwa ichangie walau asilimia 40 ya Pato la Taifa (GDP) ifikapo mwaka 2025 huku kipato cha kila mwananchi kikiwa zaidi ya Dola 3,000 za Kimarekani (zaidi ya Sh6.75 milioni) kwa mwaka au walau Sh562,500 kwa mwezi.

Kufanikisha malengo hayo yote, ni lazima uwekezaji wa kina ufanyike ndani ya muda uliopo. Uwekezaji huu nilazima ushirikishe sekta binafsi pamoja na Serikali pia.

Sekta binafsi, pamoja na vyanzo vingine, inazitegemea taasisi za fedha ambazo zimekuwa mstari wa mbele kutoa mikopo kwa wajasiriamali waweze kuanzisha viwanda au kufanya biashara mbalimbali zenye uhusiano na sekta ya viwanda.

Hata hivyo, wadau wa sekta hiyo wanasema kiasi kinachohitajika kufanikisha kujenga uchumi wa viwanda ni kikubwa kuliko uwezo uliopo.

Suala la mtaji ni moja ya mambo yaliyoibuliwa kwenye jukwaa la fikra lililoandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) na kufanyika Oktoba 4 jijini Dar es Salaam na kurushwa katika kituo cha runinga cha ITV na Radio One.

Taasisi za fedha

Akichangia mjadala huo, mkuu wa kitengo cha wateja wakubwa wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi alisema licha ya benki za biashara kutoa mikopo kwa ajili ya viwanda vidogo na vikubwa, bado kuna changamoto zinazopunguza uwezo wa kufanikisha malengo makubwa yaliyopo.

Alisema kujenga viwanda kunahitaji zaidi ya Sh48. “Hiyo ni fedha nyingi sana hata ukichanganya akiba ya benki kubwa tatu nchini haiwezi kufikia kiasi hicho,” alisema.

Mponzi alisema benki ya biashara nchini zinategemea amana za muda mfupi hivyo kutokuwa na uwezo wa kutoa mikopo ya muda mrefu mfano ya ujenzi wa viwanda.

Hata hivyo, ili kukabiliana na hali hiyo anasema ni vyema benki za biashara nchini zikashirikiana na taasisi za fedha za kimataifa kukabili changamoto hiyo.

Anasema kwa miaka mitatu benki ya NMB ikishirikiana na taasisi hizo za kimataifa imeweza kutoa Sh500 bilioni na kuzielekeza kwenye viwanda

Mchangiaji mwingine, Farkhia Walsami alisema wananchi wengi hawana mtaji na uwezo wa kuandika mpango mkakati wa biashara ambao ni miongoni mwa vigezo vinavyohutajika kabla taasisi za fedha hazijatoa mkopo.

Walsami alishauri iundwe taasisi itakayoshughulikia taasisi ndogo na namna ya kuwawezesha vijana wanaoanzisha biashara kupata mkopo bila masharti makubwa yanayokatisha tama.

“Uwe mpango maalumu usio na mahitaji ya dhamana zisizohamishika kama ardhi. Iangalie namna ya kuendeleza biashara na mawazo ya sekta,” alisema Walsami.

Hata hivyo, Mponzi alimwondoa hofu Walsami kwa kusema tayari baadhi ya benki ikiwamo NMB zimeanza kutoa mikopo ya kuanzia Sh1 milioni hadi Sh50 milioni kwa kutumia dhamana zisizo rasmi.

“Hapa mjasiliamali haitaji kuwa na mpango mkakati wa biashara ili apate mkopo huu bali maofisa wetu wataokwenda kwenye biashara yake au mradi anaoufikiria na kuzungumza naye kisha kumtengenezea hesaba na kumpa mkopo wa Sh50 milioni kuanzisha kiwanda kidogo,” alisema Mponzi.

Serikali

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage aliyekuwa mgeni rasmi katika mjadala huo alieleza jinsi Serikali ilivyojipanga kujenga uchumi wa viwanda na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Waziri alisema Serikali imeyachukua mawazo yaliyotolewa na wadau kuchochea maendeleo hasa ujenzi wa viwanda nchini.

“Nawaambia Watanzania, safari hii bado ni ndefu na ni muhimu. Mwanzoni nilisema ni dimbwi, kimsingi siyo bali ni bahari yenye mtikisiko lakini mabaharia wa kweli ni sisi,” alisema Mwijage.

Waziri huyo alisema viwanda vinavyokusudiwa ni vidogo ambavyo wmailiki wake watakuwa wanaviendeleza kadri mapato yao yanavyoongezeka na kuvikuza.

Alisema hakuna Taifa lililoendelea ambalo lilianza kujenga viwanda vikubwa isipokuwa, kwa sera na mazingira rafiki, lilijenga viwanda vidogo ambavyo leo hii vimekuwa viubwa vikuza bidhaa zake maeneo tofauti duniani.

“Tunaposema viwanda usiwaze kama cha Wazo Hill. Ukifany ahivyo, utakufa hujafanikiwa kukijenga. Tuanze kwa viwanda vidogo,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz