Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyanzo imara vya mtaji vinahitajika kufanikisha ujenzi uchumi wa viwanda

19508 Pic+viwanda TanzaniaWeb

Thu, 27 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati msisitizo mkubwa ukielekezwa kwenye ujenzi wa viwanda, upatikanaji wa mtaji kufanikisha azma hiyo ni changamoto inayowakabili wajasiriamali wengi nchini hivyo kuhitaji mkakati wa haraka kubaliana nayo.

Kufanikisha ndoto hiyo, taarifa za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonyesha zaidi ya Sh32 trilioni zinahitajika huku sekta binafsi ikipewa nafasi kubwa zaidi kuchangia katika mpango huo.

Hali ikiwa hivyo, ripoti ya Benki Kuu (BoT) inaonyesha kushuka kwa mikopo inayotolewa na benki za biashara kwa wajasiriamali ndani kwa miaka ya hivi karibuni.

Ingawa sekta ya viwanda hasa vya uzalishaji mali imeonyesha kuongeza tija, upatikanaji wa mtaji kwa ajili ya kuimarisha operesheni, ubora wa bidhaa na utafiti wa masoko mapya ni tatizo wanalokabiliana nalo wamiliki wengi.

Ripoti ya tathmini ya kila mwezi ya BoT inadhihirisha mwenendo huo unaotia mashaka kufanikisha mpango uliopo mbele ya Watanzaia wote.

Taarifa ya BoT ya Julai inaonyesha mikopo mingi iliyotolewa na benki za biashara na taasisi za fedha nchini ilikuwa binafsi ikielekezwa zaidi kwa wafanyakazi na watumishi.

Ripoti hiyo inaonyesha, kwa mwaka ulioishia Juni, zaidi ya robo ya mikopo yote iliyotolewa, asilimia 27.4, ilikuwa ya watu binafsi ikifuatiwa na biashara kwa asilimia 20.5.

Mikopo kwa ajili ya viwanda ilishika nafasi ya tatu ikiwa na asilimia 10.5 ikishuka kutoka asilimia 11.4 zilizokuwapo kwa mwaka ulioishia Juni 2017. Hata hivyo, sekta inakua na mchango wake kwenye uchumi unaongezeka kila siku.

Tathmini ta benki hiyo inaonyesha sekta ya viwanda ilikua kwa wastani wa asilimia 7.8 mwaka 2016 ikiimarika kutoka asilimia 6.5 mwaka 2015. Ukuaji mkubwa zaidi ulikuwa kwenye viwanda vya chakula, saruji, vinywaji baridi, tumbaku na nguo.

Pamoja na mwenendo huo, ajira pia ziliongezeka. Ripoti inasema kulikuwa na ajira mpya 95,678 mwaka 2016 zikilinganishwa na 91,008 zilizokuwapo mwaka uliotangulia.

Zaidi ya nusu ya ajira hizo zilipatikana kwenye viwanda vya vyakula, vinywaji baridi na tumbaku.

Mikopo ya muda mrefu

Tofauti na sekta nyingine, changamoto zinazovikabili viwanda kukopesheka kwenye benki za biashara na taasisi za fedha huchangiwa na mfumo wa ukopeshaji na uendeshaji wa viwanda vyenyewe.

Benki nyingi, inaelezwa kuwa hujielekeza zaidi kwa wateja wanaochukua mikopo ya muda mfupi jambo lisilowezekana kwenye mahitaji ya viwanda ambavyo mchakato wake wa uzalishaji una mlolongo mkubwa kidogo.

Mchumi na mtafiti mwandamizi, Profesa Samwel Wangwe anasema benki nyingi nchini haziwezi kutoa mikopo ya muda mrefu inayohitajika zaidi viwandani kwa sababu zinategemea amana za wateja wao.

“Fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo hutegemea zaidi mikopo ya muda mrefu ambayo hupatiakana kutokana na mtaji wa Serikali au fixed deposits (amana za muda maalumu). Nchini, benki zinategemea amana kukopesha,” anabainisha msomi huyo.

Kutokana na ukweli huo, anasema Benki TIB Development inapaswa kuwa na mchango mkubwa zaidi katika utekelezaji wa ajenda ya viwanda.

Msimamo wa mchumi huyo unaungwa mkono na mwenzake wa Chuo Kikuu cha Zanziar, Profesa Haji Semboja anayesema kukosekana kwa mikopo ya muda mrefu kunakwaza uanzishaji wa viwanda vipya na uendelezaji wa vilivyopo.

Anawapa changamoto watunga sera na watendaji wa sekta ya fedha nchini kuangalia namna ya kuachana na mfumo wa benki nyingi kuwaangalia zaidi wafanyakazi na watumishi badala ya miradi yenye mchango kwa maendeleo ya jamii kubwa zaidi.

“Miradi ya maendeleo inahitaji mikopo ya muda mrefu wakati benki zetu zinapenda zaidi kuwakopesha watumishi. Hapa ndipo tunapohitaji kupafanyia kazi,” anasema Profesa Semboja.

Kinachozikimbiza benki nyingi kutoa mikopo ya muda mrefu ni hatari ya miradi mikubwa kutotekelezwa kama ilivyopangwa. Taasisi nyingi huogopa kuzichangamkia kampuni zinazotekeleza miradi hiyo kwa hofu kuwa endapo zitafilisika nazo zitakuwa zimepoteza fedha zilizokopesha.

Ofisa mtendaji mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), Moremi Marwa anasema kuna fursa ambayo wajasiriamali wengi nchini hawajaitumia ipasavyo.

Si sekta binafsi pekee ambayo haijaiona na kuipa kipaumbele, anasema hata Serikali inayojenga miradi mikubwa ya maendeleo bado inatumia zaidi fedha zake au mikopo kutoka vyanzo tofauti.

“Serikali inatekeleza miradi mingi ya maendeleo lakini hakuna hata mmoja uliopata fedha kutoka DSE. Tunaiomba iangalie uwezekano wa kutoa (amana za miundombinu) infrastructure bond ili kukuza uwezo wa soko letu,” anasema Moremi.

Serikali inajenga miradi mingi ya maendeleo kwa mfani ni reli ya kisasa (SGR), mradi wa umeme wa Stigler’s Gorge, mpango wa elimu bila malipo na usambazaji wa umeme vijijini (Rea) huku sekta binafsi ikitakiwa kuanzisha viwanda vya kuchakata malighafi zinazozalishwa maeneo tofauti.

Kufanikisha hilo, anasema ipo haja ya kuwa na vyanzo imara vya mtaji kutoka ndani hata nje ya nchi pamoja na usimamizi makini wa kutekeleza miradi inayokusudiwa.

“Tunahitaji kuwa na taasisi imara za fedha zitakazotoa mtaji kwa miradi yetu…watu wenye ujuzi, teknolojia ya kisasa na masoko ya uhakika kwa bidhaa tutakazozalisha,” anasema Marwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz