Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyama vya ushirika vyahudumia 229,000

VYAMA.jpeg Vyama vya ushirika vyahudumia 229,000

Wed, 6 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

JUMLA ya wateja 229,000 wamekuwa wakihudumiwa na vyama vya ushirika mkoani Mbeya kwa lengo la kujiongezea kipato kutokana na fursa mbalimbali ambazo wamekuwa wakipata zikiwamo za usimamizi bora wa soko la mazao yao.

Hayo yalielezwa jana na Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoani Mbeya, Angela Maganga, wakati akizungumza gazeti hili kuhusiana na hali ya ustawi wa ushirika mkoani hapa kwa vyama vya ushirika.

Alisema Vyama vya Msingi vya Kilimo na Masoko (AMCOS) ambavyo vimekuwa vikisimamia mazao kama kakao, tumbaku na kahawa, vimekuwa na mchango mkubwa katika kusimamia masoko ya uhakika ya wakulima katika soko, hivyo kuleta manufaa ya kiuchumi kwa wakulima wanaouza mazao yao.

Akitolea mfano kwa zao la kokoa, Angela alisema bei ya zao hilo imepanda kutoka Sh. 1500 hadi kufikia Sh. 5,000 hadi sasa kutokana na wakulima wengi kujenga utamaduni wa kuuza zao hilo kwenye vyama vya ushirika.

“Hadi kufikia Desemba 2019 wakulima waliweza kuuza kakao kwenye vyama vyao vya ushirika na kupata kiasi cha Sh. bilioni 59.8 na kuwa wengi wa madalali wameanza kuacha kazi hiyo ya udalali kutokana na kutokuwa na manufaa,” alisema Angela.

Alisema zao la tumbaku mpaka sasa kuna vyama 17 vya ushirika na kuwa kwa msimu wa mwaka jana jumla ya kilo milioni 11 ziliuzwa kupitia vyama hivyo vya ushirika na kuwa kiasi cha Sh. bilioni 40 zilipatikana na kugawiwa kwa wakulima hao.

Alisema uwapo wa vyama vya ushirika umekuwa ni mkombozi mkubwa kwa watu wengi hususan wakulima kutokana na kuwapo kwa changamoto ya wakulima wengine kuuza mazao yao kwa madalali ambao wamekuwa wakinunua mazao kwa bei ya dezo ambayo yamnufaishi mkulima.

Alisema mkoa wa Mbeya una jumla ya Saccos 212 ambazo zina hisa za Sh. bilioni 16, akiba kiasi cha Sh. bilioni 19 na Amana kiasi cha Sh. bilioni tano.

Alisema mikopo iliyotolewa kwenye Saccos hizo ni kiasi cha Sh. bilioni 64 na kuwa kati ya mikopo hiyo iliyotolewa kuna kiasi cha Sh. bilioni 40 ambazo zimerejeshwa mpaka sasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live