Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyama vya ushirika sasa kuendeshwa kidigitali

2db19f1c520c7313c837ccd7e09d9272 Vyama vya ushirika sasa kuendeshwa kidigitali

Fri, 6 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini (TCDC), imejipanga kufanya usajili na ufuatiliaji wa uendeshaji wa Vyama vya Ushirika Nchini ( AMCOS) kwa njia ya mtandaoni, ili kudhibiti ufujaji wa mali za ushirika.

Hayo yamebainishwa na Mrajis wa TCDC, Dk. Benson Ndiege, alipokuwa akizungumuza na waandishi wa habari katika kongamano la wanawake mkoani Geita kulenga kuhamasisha uundwaji wa madirisha na ushirika wa wanawake.

Dk. Ndiege amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kubaini upotevu holela wa mali za ushirika kwenye maeneo mengi, hali iliyotishia uhai wa vyama vya ushirika na hata kupoteza mali za umma na wanachama kutonufaika.

“Tunaondoka kwenye boksi, ule ushirika wa mazao tuliokuwa tunafanya, tunaenda kwenye ushirika wa kidigitali, ushirika ambao unaendana na shughuli, unaendana na umri, unaendana na aina ya watu hao,” amesema na kuongeza kuwa:

“Tunakuja na mfumo wa kielektroniki, ambao sasa vyama vyote vya ushirika vitatambulika, vitasajiliwa kwenye mfumo, mali zake zitasajiliwa kwenye mfumo, wanachama wake watasajiliwa kwenye mfumo, mwisho wa siku usimamizi ule utakuwa wa wazi zaidi, kuliko sasa hivi”.

Dk. Ndiege amebainisha hadi sasa kuna jumla ya Amcos 9,471 ambazo zimesajiliwa nchi nzima, huku vingi vikiwa bado vinaendeshwa kwa mfumo wa kizamani na uliojikita zaidi kwa wakulima na siyo makundi mengine.

Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo Wanawake Geita, (GEWOMA), Asia Masimba amesema mpango mpya wa usajili na uendeshaji wa Amcos utasaidia kundi la wachimbaji wanawake kupata mitaji na vitendea kazi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule ametoa wito kwa wanawake watakaounda Amcos kujiendesha kwa weledi, ushirikiano na uaminifu, ili Amcos ziwe madaraja ya kujikwamu kiuchumi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live