Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vodacom yamtangaza bosi mpya Mtanzania

Vodacompiic Data Vodacom yamtangaza bosi mpya Mtanzania

Tue, 5 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania, imemtangaza Hilda Bujiku kuwa kaimu mkurugenzi mtendaji akichukua nafasi ya Sitholizwe Mdlalose aliyedumu kwenye nafasi hiyo kwa miezi 10.

Mdlalose aling’atuka kwenye nafasi hiyo baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi mtendaji wa Vodacom nchini Afrika Kusini.

Hilda anapokea kijiti akiwa ni Mtanzania na mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo katika kampuni hiyo ikiwa ni miezi saba tangu bodi ya wakurugenzi imteue kuwa mkurugenzi wa fedha Novemba, mwaka 2021.

Taarifa iliyotolewa kwa umma na Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Vodacom, Jaji mstaafu Thomas Mihayo ilieleza Hilda atashika nafasi hiyo hadi pale taratibu za kumpata mkurugenzi mpya utakapokamilika.

Jaji Mihayo alimpongeza Hilda kwa hatua hiyo huku akiwataka Watanzania kuendelea kufanya kazi kwa juhudi, ili kushika nyadhifa za juu za uongozi kwenye kampuni na taasisi kubwa.

“Inaleta faraja kuona Watanzania wanashika nafasi za juu kama hivi, uchapakazi ndiyo msingi wa kila kitu, hivyo niwasihi Watanzania wafanye kazi kwa bidii, kwani uwezekano wa kupata nafasi hizi upo,” alisema Jaji Mihayo.

Uteuzi huo wa Hilda ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha ulianza Julai mosi mwaka huu.

Kabla ya uteuzi huo, Hilda aliyejiunga na kampuni hiyo mwaka 2012 amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika kampuni hiyo ikiwemo naibu mkurugenzi wa fedha anayehusika na mipango na uchambuzi.

Mbali na Tanzania, Hilda aliwahi kufanya kazi kama mkurugenzi wa fedha wa kampuni ya Vodacom nchini Lesotho na kufanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali iliyoongeza tija kwenye kampuni hiyo.

Kulingana na taarifa hiyo ya Jaji Mihayo, Hilda atakaimu nafasi ya mkurugenzi mtendaji wakati akiendelea na majukumu yake kama mkurugenzi wa fedha hadi pale taratibu za kumpata mkurugenzi mtendaji zitakapokamilika.

Katika nafasi ya ukurugenzi wa fedha, Hilda amekuwa akiongoza mchakato wa bajeti kulingana na mkakati wa kampuni na kuendesha programu ya uwekezaji inayolenga kupata wawekezaji wapya huku ikiendelea kuwalinda wawekezaji waliopo.

Miongoni mwa majukumu yake ni kuhakikisha kampuni inazingatia soko la hisa na sheria na kanuni za dhamana za soko la mitaji.

Kitaaluma, Hilda ana Shahada ya Kwanza ya Biashara ya Uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Pia amekamilisha kwa ufanisi programu ya uongozi inayotolewa na kampuni ya Vodacom.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live