Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viwanja Sabasaba sasa kugeuzwa soko endelevu

10235 Saba7+pic TZW

Thu, 28 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tayari suala hilo lipo kwenye mchakato ili kuhakikisha linatekelezeka

Dar es Salaam. Mwenyekiti Bodi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade), Christopher Chiza amesema viwanja vya Sabasaba vitageuzwa kuwa soko endelevu baada ya maonyesho ya mwaka huu.

Alisema hayo jana alipokuwa akitoa tathmini ya maandalizi ya maonyesho hayo ya 42 yatakayofanyika kwa siku 16 mfululizo kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.

“Tumetoa mapendekezo ya kuvigeuza viwanja hivi kuwa soko endelevu baada ya maonyesho ili kuwapa fursa wafanyabiashara wetu kuendelea kuonyesha na kuuza bidhaa zao humu badala ya kufunga mabanda,” alisema Chiza.

Alifafanua kuwa tayari suala hilo lipo kwenye mchakato ili kuhakikisha linatekelezeka baada ya maonyesho haya kuisha.

Chiza alisema masuala yote ya msingi yatazingatiwa ili kuhakikisha usafi na usalama ndani ya viwanja unakuwapo siku zote.

Hata hivyo, akizungumzia maonyesho hayo ya 42 alisema wanalenga zaidi kutatua changamoto za wafanyabiashara.

“Kumekuwa na changamoto za wafanyabiashara wadogo, wakubwa na wakati. Kubwa ni suala la usajili wa majina ya biashara. Taasisi zinazohusika kama vile Nida, TFDA, Sido wamekuwa wakilalamikiwa katika kutoa uthibitisho kwa lengo la kusajiliwa,” alisema.

Alisema suala la vitambulisho vya Taifa pia limekuwa ni changamoto kwa sasa katika usajili wa makampuni na majina ya biashara,” alisema.

Chiza alisema wafanyabiashara wengi wanalalamika vinatolewa kwa tabu jambo linalochelewesha usajili.

Alisema maonyesho yanalenga zaidi kutatua changamoto kama hizo na kuona ni kwa namna gani wafanyabiashara watapewa nafasi kusajiliwa biashara zao kirahisi.

Chanzo: mwananchi.co.tz