Sekta ya viwanda imeanza kupoteza mvuto katika soko la ajira nchini kutokana na mageuzi ya teknolojia, ripoti imebaini huku wachumi wakisema inapaswa kuwa kinyume chake.
Idadi kubwa ya vijana sasa wanahamia sekta ya kilimo na huduma zinazotajwa kuwa na fursa nyingi ikilinganishwa na viwanda.
Ripoti ya utafiti wa kufuatilia mwenendo wa mahitaji ya kaya (NPS) ya mwaka 2020/21, inayoonyesha watu ndani ya miaka sita iliyopita, watu sita kati ya kumi waliokuwa wameajiriwa sekta ya viwanda wamehamia kwenye kilimo na huduma.
Ripoti hiyo inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza hadi mwaka 2021 asilimia 81.4 ya nguvu kazi nchini ilikuwa inajishughulisha na kilimo.
Asilimia 31.3 ya nguvu kazi iliyokuwa sekta ya viwanda mwaka 2014/15, imehamia huko huku asilimia 31.9 ikihamia sekta ya huduma.
Hata hivyo, mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa (GDP) umeendelea kukua mfululizo kutoka asilimia saba mwaka 2019 hadi asilimia nane mwaka 2021 wakati huo mchango wa kilimo umeporomoka kwa asilimia kumi kati ya mwaka 2020 na mwaka 2021.
Kuhusu hali hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Viwanda ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Lugano Wilson alisema hiyo ni changamoto inayoweza kusababisha kudorora kwa uzalishaji katika sekta hiyo, kuathiri tija na kusababisha uhaba wa mahitaji muhimu.
“Upungufu wa nguvu kazi utasababisha uzalishaji kudorora. Hali hiyo itaathiri tija ya viwanda, kwani bidhaa husika hazitaweza kukidhi mahitaji ya ndani na ya nje,” alisema
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la wenye viwanda Tanzania (CTI), Hussein Suphian alisema teknolojia imeleta mageuzi hayo, akitoa mfano wa kiwanda cha ngano cha kampuni za Bakhresa, Buguruni kimepunguza wabeba mizigo kutoka 30 hadi kubakia wanne.
“Si hicho tu, kiwanda cha saruji Dangote, mkoani Mtwara hakina vijana wabeba saruji ila ni mitambo tu, hata kiwanda cha sukari Bagamoyo kina mageuzi makubwa sana ya ‘automations’, lakini viwanda vya zamani vingi vinaendelea kutumia teknolojia za zamani,” alisema.
Tatizo la kimfumo
Profesa Abel Kinyondo kutoka Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema mazingira hayo ya ukuaji usio halisi huathiriwa na sababu mbalimbali ikiwamo mageuzi ya teknolojia au vikwazo vya uzalishaji unaoathiri ajira zilizopo.
“Kadri uchumi unavyozidi kukua, ndivyo idadi kubwa ya nguvu kazi inahama kutoka sekta ya kilimo kwenda katika sekta ya huduma, lakini Tanzania imekuwa kinyume chake kutokana na mazingira magumu ya uwekezaji sekta ya viwanda, sioni kama ni teknolojia,” alisema.
Alisema ukuaji halisi wa uchumi huanza kupunguza ajira sekta ya kilimo inayohamia viwandani kutokana na athari za mageuzi ya teknolojia kuanzia uzalishaji, viwandani hadi sekta ya huduma kwa mtiririko wa athari hizo za kiteknolojia.
“Lakini takwimu hizi zinaonyesha kinyume chake, yaani nguvu kazi kubwa inahamia kwenye kilimo ambako ndio ilitakiwa kuonekana ikipungua kwa sasa.Kwa mfano tungeona mkulima anatumia teknolojia kuzalisha mazao bila watu wengi,” alisema Profesa Kinyondo.
Mtaalamu wa uchumi na biashara, Dk Donath Olomi alisema kati ya mwaka 2016 hadi 2020 hakukuwa na mwelekeo mzuri wa taasisi za kifedha kuwezesha mikopo viwandani.
Dk Olomi alisema shughuli za viwanda ziliathiriwa na mfumo wa Serikali ya awamu ya tano uliosababisha ajira kuporomoka kutokana na utitiri wa kodi, ukamataji na vitisho.
“Ukusanyaji wa kodi ulijaa vitisho, hata mikopo ilipungua kwenye sekta ya viwanda kutokana na mazingira yasiyokuwa na uhakika wa kibiashara, sekta ya huduma haina mchango mkubwa katika GDP kwa hiyo si ya kujivunia,” alisema.
Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2022 inaonyesha kulikuwa na upungufu wa mahitaji ya mikopo sekta ya viwanda kwa wastani wa asilimia nne ya mikopo misimu wa 2015/16, mwaka 2017/18 na 2020/21 huku ikipata asilimia 3.2 mwaka 2019/20.