Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vivutio vya utalii Tanzania kutangazwa katika viwanja vya ndege 40 duniani

Vivutio vya utalii Tanzania kutangazwa katika viwanja vya ndege 40 duniani

Fri, 22 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tanzania itatangaza vivutio vyake vya utalii katika viwanja vya ndege 40 duniani bure katika kumbi za kupumzika na magari ambayo yanahudumia abiria.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kuingia mkataba na kampuni inayoshughulikia huduma za ndege, abiria na magari kwenye viwanja vya ndege (NAS) ambao watafanya na Serikali ya Tanzania kwa miaka mitatu.

Akizungumza leo Alhamisi Novemba 21, 2019 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Dk Hamisi Kigwangalla amesema sekta ya utalii inaingiza asilimia 20 ya fedha za kigeni nchini kwa hiyo ni lazima kuitangaza nchi mbalimbali duniani kuongeza idadi ya watalii.

"Ni sekta inayoongoza kuleta fedha zaidi za kigeni nchini, kwa hiyo ili sekta ikue na kuleta mchango tunaohitaji lazima tufanye uwekezaji," amesema Dk Kigwangalla

Amesema ufufuaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ni moja ya hatua kubwa ya kuinua sekta ya utalii nchini ili waweze kufika katika vituo vilivyopo na vitakavyotangazwa.

Mwenyekiti wa TTB, Jaji mstaafu Thomas Mihayo amezitaka kampuni na wadau wa utalii kuweka bei za vifurushi wanavyotoa kwa huduma za kitalii ili pindi watakapoenda kutangaziwa katika viwanja vya ndege vya kimataifa watalii kujua ni bei gani na wapi panawafaa na sio kutangaza tu majina peke yake.

Jaji Mihayo amesema bodi hiyo ina jukumu la kutafuta masoko ndani na nje na upatikanaji wa masoko utakuwa na tija kwenye kukuza utalii.

Naye Mkurugenzi wa Bodi ya NAS Afrika, Balozi Costa Mahalu amesema kampuni hiyo inafanya kazi katika nchi 17 Afrika, Asia na Mashariki ya Kati watahakikisha vivutio vya Tanzania vinatangazwa katika nchi zote wanazofanyia kazi na kwa kuanzia nchini wameleta basi la kubeba abiria lenye picha za mbuga za wanyama mbalimbali.

NAS ambayo imetoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 360 imetoa huduma kwa ndege zaidi ya 8,500 kwa mwaka 2019 na taarifa kuhusu Tanzania zitafikia watu wengi duniani.

"Kwa Tanzania tunafanya kazi katika viwanja vya ndege vya Dar es Salaam, Dodoma na Kilimanjaro ambapo tutapeleka mabasi ya kuhamasisha utalii na kuutangaza," amesema Balozi Mahalu

Chanzo: mwananchi.co.tz