Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vivo Energy yapania kuteka soko vilainishi

Vivoen Vivo Energy yapania kuteka soko vilainishi

Sat, 13 Nov 2021 Chanzo: Nipashe

KAMPUNI ya Nishati ya Vivo Energy Tanzania, wauzaji na wasambazaji wa vilainishi vya kampuni ya Shell na Engen imerejesha nchini vilainishi hivyo na kuwataka Watanzania kuvitumia kwa usalama wa magari yao, ikitamba kuwa ni rafiki wa mazingira.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa vilainishi vya Shell, Meneja Biashara wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Kemilembe Kafanabo, alipongeza jitihada za kampuni hiyo kwa juhudi zake za kusambaza bidhaa zenye ubora wa hali ya juu zenye manufaa kwa umma na jamii zikilenga sio tu kuongeza utendaji kazi wa magari na mitambo mingine lakini pia inalinda mazingira.

“Kama EWURA, tunatamani kuona vilainishi vinavyosambazwa nchini vinakidhi viwango vilivyowekwa. Kwa kufanya hivyo, tunalinda maslahi ya watumiaji na wananchi.

"Ili kuhakikisha bidhaa zinazosambazwa zinakidhi viwango vinavyotakiwa, EWURA inategemea kuanza kusajili vilainishi vyote vinavyosambazwa nchini. Hii ni pamoja na kuwasajili Vivo ambao wameidhinishwa kusambaza vilainishi vya Shell. hatua itakayopunguza usambazaji wa bidhaa ghushi nchini,” alisema Kafanabo.

Alisema kuwa mamlaka hiyo iko tayari kufanya kazi bega kwa bega na waendeshaji wa kampuni hiyo ili kuboresha zaidi mazingira ya biashara ya vilainishi na kuhakikisha vitega uchumi vya jamii vinalindwa na watumiaji wanapata bidhaa zinazokidhi viwango vinavyotakiwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Vivo Energy Tanzania, Khady Sene, alibainisha kampuni hiyo imeamua kuingia mkataba wa kusambaza vilainishi vya Shell kutokana na umahiri wake kwenye uzalishaji wa vilainishi duniani.

Alisema kuwa teknolojia inayotumiwa na kampuni ya Shell ni ya kisasa inayokidhi matakwa ya kitaalamu, ikichangiwa na uwapo wake wa muda mrefu sokoni huku ikiaminiwa na kutumiwa na kampuni kubwa za magari na nyinginezo kubwa zinazohitaji huduma ya vilainishi.

Alisema ipo zaidi ya nchi 100 na Tanzania imefurahi kuwa kati ya nchi hizo na Vivo Energy Tanzania ndiyo wasambazaji pekee wa vilainishi hivyo nchini," alisema.

Mtaalamu wa Ufundi wa Vivo Energy, Fred Omondi alibainisha kuwa vilainishi vya Shell vitakavyokuwa vikiuzwa Tanzania ni hivyo hivyo vinavyouzwa nchi nyingine kubwa duniani kwa ubora na ufanisi wake.

“Tuna vilainishi vya aina tatu kama vile Shell Rimula kwa ajili ya mashine kubwa kubwa, Shell Helix kwa magari ya abiria na Shell Advance kwa ajili ya pikipiki," alifafanua Omondi.

Chanzo: Nipashe