Jumla ya wakulima 2,001 kisiwani Pemba wamesajiliwa kunufaika na mradi wa Viungo, Mboga na Matunda katika kipindi cha mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mradi huo kati ya wakulima 2,175 ambao walilengwa kufikiwa na kusajiliwa katika kipindi hicho cha utekelezaji wa mradi.
Hayo yamebainishwa na meneja uendeshaji mradi huo kanda ya Pemba, Sharif Maalim Hamad wakati akiwasilisha tathimini ya utekelezaji wa mradi huo katika mkutano na wataalam wa kilimo pamoja na wakulima viongozi uliolenga kujadili mafanikio na changamoto za utekelezaji wa mradi katika kipindi cha mwaka wa kwanza.
Alitaja wanawake kuwa ndio walionufaika zaidi katika kipindi hicho ikilinganishwa na wanaume ambapo jumla ya wanawake 1,211 walisajiliwa kunufaika huku wanaume wakiwa ni 790.
“Katika kipindi cha mwaka wa kwanza tumefanikiwa kusajili idadi kubwa ya wanawake ikilinganishwa na wanaume na hii ni kutokana na kwamba mradi umetoa kipaumbele sana kwa wanawake,” amesema Hamad.
Kwa upande wake meneja mkuu wa mradi huo Amina Ussi Khamis aliwataka maafisa kilimo kushirikiana pamoja kutatua changamoto zinazowakabili wakulima ikiwa ni pamoja na kutoa taaluma sahihi za uzalishaji ili kusaidia lengo la mradi liweze kufikiwa katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi huo.
“Mradi utaendelea kuwasaidia wakulima katika maeneo mbalimbali ikiwemo utoaji wa taaluma ya uzalishaji bora wa mazao na pembejeo lakini pia wakulima wanalo jukumu la kendelea kuchangia nguvu katika baadhi ya maeneo ili kurahisisha upatikanaji wa matokeo kwa haraka,”amesema Bi.Amina.
Wataalam wa kilimo wamesema utekelezaji wa mradi kisiwani Pemba umesaidia kuongeza hamasa kwa wakulima kujikita katika kilimo hicho kutokana na taaluma ambayo inatolewa kupitia shamba darasa zilizoanzishwa kwenye shehia ambazo mradi unatekelezwa