Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vituo vipya vya mafuta vyatakiwa kuwa na sehemu ya gesi asili

3bfd433ec94b97f92dce5b23f8dcf106 Vituo vipya vya mafuta vyatakiwa kuwa na sehemu ya gesi asili

Sat, 26 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Nchi, Ofi si ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo amelitaka Baraza la Taifa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuhakikisha vituo vyote vipya vya mafuta vinazingatia uwapo wa sehemu iliyotengwa kwa ajili ya gesi asilia ndipo litoe cheti cha usajili.

Jafo ametoa agizo hilo leo kwa Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka kwenye hafla iliyoandaliwa na kampuni ya magari ya Scania ya uzinduzi wa gari linalotumia mfumo wa gesi asilia Dar es Salaam.

“Umefika wakati sasa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa upande wa mazingira tunapotoa vyeti vya mazingira kwa ajili ya vituo vya mafuta ni lazima vituo hivyo viwe na sehemu maalumu ya kuwekea gesi asilia ili kurahisisha upatikanaji wa gesi itakayotumika kwenye magari yanayotumia gesi hiyo,” alisema.

Jafo alisema endapo Tanzania itatumia gesi asilia kwenye magari itakuwa ni hatua kubwa katika utunzaji wa mazingira hasa kwenye eneo la kuzuia uchafuzi wa hewa na uchafuzi wa kelele unaosababishwa na magari yanayotumia mafuta ya dizeli na petroli. Kwa mujibu wa Waziri Jafo, zaidi ya ujazo wa trilion 57.54 za gesi zinapatikana nchini lakini matumizi yake bado hayajafikia ujazo wa trilion moja.

“Naomba wawekezaji kutumia fursa hii kuwekeza kwenye nishati hii kwasababu ipo ya kutosha na tutaepuka gharama zisizo za lazima kuagiza mafuta nje ya nchi,” alisema.

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema Tanzania inaongoza kwa gesi nyingi ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki . Alisisitiza gesi ni utajiri mkubwa unaohitaji uwekezaji makini utakaoleta manufaa ya kiuchumi katika nchi .

Kalemani alisema, umeme unaotumika nchini ni zaidi ya asilimia 70 unatokana na gesi asilia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), James Mataragio aliwahakikishia wawekezaji wa gesi kuwa serikali kupitia shirika hilo inachukua hatua mbalimbali kwa ajili kuhakikisha gesi inayopatikana inasambazwa maeneo mbalimbali hasa viwandani na majumbani.

Chanzo: www.habarileo.co.tz