Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vitambulisho vya wajasiriamali vyampaisha JPM

79d5f9d93515506d7e3b0a684add299d.jpeg Vitambulisho vya wajasiriamali vyampaisha JPM

Sat, 29 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI ya Awamu ya Tano imefanikiwa kuweka mazingira bora kwa wajasiriamali wadogo hatua ambayo imetajwa na wadau mbalimbali kwamba imedhihirisha kwamba ipo kwa ajili ya wanyonge na ina nia ya dhati ya kupunguza umasikini .

Utoaji wa vitambulisho maalumu kwa wajasiriamali kwa gharama nafuu, mikopo kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu, ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwamo vituo vya mabasi, ni miongoni mwa mambo yanayompaisha Rais John Magufuli akitajwa kuwa ni mkombozi wa wanyonge.

Vitambulisho

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo katika mikoa mbalimbali, walisema awali walifanya shughuli zao bila uhuru lakini baada ya Magufuli kuingia madarakani, wamepewa heshima ya kutambulika na kuondokana na kero ya kukamatwa na mgambo.

Kiongozi wa wafanyabiashara ndogo, mama lishe na baba lishe wa soko kuu la Bukoba mkoani Kagera, Catherine Kagere alikiri kwamba kulikuwa na uadui mkubwa kati ya wafanyabiashara wadogo na wakusanya ushuru.

“Sitasahau mgambo walivyonimwagia matunda na kunifungia kibanda changu wakati wakinidai ushuru wa Sh 50,000…Namshukuru sana Rais Magufuli, ametukomboa kwa kutupa vitambulisho. Unalipa Sh 20,000 kwa mwaka mzima!” alisema mfanyabiashara ndogo, Tumaini Bernard (29) mkazi wa manispaa ya Bukoba.

Mwenyekiti wa mama lishe katika Mtaa wa Nyakanyasi mjini Bukoba, Rosemary Stanislaus alisema Rais Magufuli alisema, “Kama kuna mtu anabeza haya mazuri tuliyofanyiwa sisi wafanyabiashara ndogo, anapaswa kufikiriwa akili zake mara mbili kwani changamoto tulizokutana nazo miaka ya nyuma hazielezeki.”

Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera Bernard Limbe alithibitisha kwamba tangu vitambulisho hivyo vitolewe mwaka 2018, vurugu na migogoro kati ya mgambo na wajasiriamali imekoma.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Marco Gaguti, awamu ya kwanza mkoa ulipokea vitambulisho 25,000 na hadi Februari mwaka jana, vitambulisho 17,369 viligawiwa.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara katika soko la Mwanga, mjini Kigoma, Raymond Ndabiyegetse alisema vitambulisho vya wajasiliamali vimewasaidia kwa kufanya watambulike kutokana na taarifa zao kuwapo serikalini na pia vimeondoa adha ya kukimbizana mgambo.

Mfanyabiashara wa samaki katika soko la Malungu eneo la Mwanga, mjini Kigoma, Diana Samson alisema katika kukimbizana na mgambo, baadhi walijikuta wakipoteza bidhaa.

Ofisa Biashara katika Sekretarieti ya Mkoa wa Kigoma, Deo Sangu alisema nusu ya vitambulisho vilivyotolewa kwa mkoa huo vimeshauzwa kwa wajasiliamali. Kwa mujibu wa Sangu, hadi Juni 24, jumla ya vitambulisho 24,341 sawa na asilimia 50 ya vitambulisho vilivyotolewa kwa mkoa huo, vilishauzwa.

Mkoani Mwanza, baadhi ya watu wanaojishughulisha na shughuli za gereji, usafirishaji kwa bajaji, pikikipiki na baiskeli jijini Mwanza, walishukuru Rais Magufuli kwa wajali kwa kuamuru wasibughudhiwe.

“ Sidhani kama kuna mjasiriamali asiyeona mazuri ya rais wetu,” alisema Ndyanabo Tinshereka anayejishughulisha na kuziba pancha na kujaza upepo magari katika mtaa wa Mabatini.

Alipohutubia Bunge la 11 kwa mara ya mwisho, Juni mwaka huu Dodoma, Rais Magufuli alisema, mwaka jana, jumla ya wajasiliamali wadogo 1,591,085 walipatiwa vitambulisho.

“Mtakumbuka, zamani, kabla ya utaratibu huo kuanza, wajasiliamali wadogo walikuwa wakibugudhiwa sana na mgambo, ikiwemo kunyang’anywa mali zao. Hivyo, kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa vitambulisho hivyo, tumedhihirisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ipo kwa ajili ya wanyonge,” alisema Rais.

Mikopo

Serikali ilitunga sheria yenye kutaka halmashauri zote kutenga asilimia 10 ya mapato yao kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba kwa wanawake (asilimia nne), vijana (asilimia nne) na wenye ulemavu (asilimia mbili). Kwa mujibu wa Rais Magufuli, hadi Machi mwaka huu, Sh bilioni 93.2 zilikuwa zimetolewa.

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imewaandalia wajasiriamali na wafanyabiashara ndogo maeneo katika kituo kikuu cha mabasi kinachojengwa Mbezi Luis ambako eneo limetengwa kwa ajili ya wamachinga, mama lishe na baba lishe, wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana alisema kituo hicho ni mojawapo kati ya miradi mikubwa ya kimkakati ya serikali ya awamu ya tano inayotekelezwa kwa mafanikio makubwa na kunufaisha wananchi.

Mradi mwingine ni wa vituo vya kuendeleza utamaduni, utalii wa ndani ambao Mkuu wa Kitengo cha Itifaki na Uhusiano, halmashauri ya jiji, Gaston Makwembe, alisema wanawake na vijana wanaopata mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri watanufaika.

Chanzo: habarileo.co.tz