Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vitambulisho vya machinga vyadoda

Vitambulisho Pc Datadd Vitambulisho vya machinga vyadoda

Sun, 3 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Kasi ya uchukuaji wa vitambulisho vya wajasiriamali wadogo nchini imepungua, huku ikielezwa kuwa waliojitokeza kuvichukua ni chini ya asilimia 40 ya wafanyabiashara hao.

Vitambulisho hivyo vilianza kutolewa kwa wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga mwaka 2018, lakini vilisitishwa mwaka jana na kuanza kutolewa upya mwaka huu, huku vikiwa vimeongezwa kipengele cha picha ya mhusika pamoja na taarifa nyingine.

Akizungumza juzi jijini hapa, Mkurugenzi mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (Neec) Beng’i Issa alisema, miaka miwili iliyopita vitambulisho hivyo vilikuwa vikichukuliwa vyote.

“Havijafika (vilivyochukuliwa) asilimia 40 ya vile vilivyotolewa kwa sababu ya utaratibu mrefu wa kuvipata, lakini tumeona kuwa vina mabadiliko ambayo yana tija,” alisema.

Alitaja mabadiliko hayo kuwa ni kutengenezwa kwa mfumo wa kidijitali, huku vikiwa vimeunganishwa na mifumo mingine, ukiwamo ule wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Alisema vitambulisho hivyo vinalenga kuwasaidia wajasiriamali kupata mikopo au kuongezeka ufanisi katika biashara zao.

Mkoani Dodoma, Katibu tawala msaidizi (uchumi), Aziza Mumba alisema wamefanikiwa kugawa vitambulisho 1,092 kati ya wafanyabiashara 56,000 wanaotakiwa kupata.

Alisema kasi bado ni ndogo ya uchukuaji wa vitambulisho hivyo vilivyoanza kutolewa Aprili mwaka huu, lakini wanaamini wakati wa kuwapangia maeneo ya kwenda kufanya biashara watahamasisha ili watambulike.

Alisema kwa mkoa wa Dodoma benki ambayo inatoa mikopo kwa wafanyabiashara hao ni CRDB ambapo tayari kuna watu wameshanufaika.

Uwezeshaji machinga

Being’i alisema katika kongamano la uwezeshaji la kitaifa la tano litakalofanyika Oktoba 4 2021, jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, watatambua na kuipa tuzo mikoa iliyofanya vizuri katika eneo la machinga, ikiwamo kuwaweka katika mazingira wezeshi ya biashara.

“Tunaangalia mkoa ambao umejipanga vizuri, ikiwamo kutatua changamoto ya maeneo ya wamachinga. Kuna mikoa ambayo imefanya vizuri sana baada ya kuiona hii changamoto muda mrefu na kuamua kutenga maeneo,” alisema.

Alisema kuna mikoa ambayo imetenga maeneo na machinga wameenda kukaa kwenye maeneo waliyowekewa, huku mikoa mingine wengine ikiwasaidia kuanzisha vyama vya ushirika na kuwapa mikopo.

Chanzo: mwananchidigital