Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vitalu vya tumbaku hatarini kukauka kwa ukame

Ukamee Data Vitalu vya tumbaku hatarini kukauka kwa ukame

Wed, 2 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Uhaba wa maji katika katika maeneo mengi nchini, unahatarisha hata ukuaji wa vitalu vya miche ya tumbaku na hivyo kuhatarisha uzalishaji wa tumbaku kufikia kilo milioni mia moja msimu huu kama hali hiyo haitadhibitiwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku nchini, Stan Mnozya akitembelea vitalu vya miche ya tumbaku jana Jumanne Novemba 1, 2022 Wilaya ya Uyui, amesema hali ni mbaya kwa vile hakuna maji.

"Ukame unahatarisha hali ya miche katika vitalu hii ni hatari kama hali itaendelea hivi," amesema.

Ameeleza kuwa, miche inapaswa iwe mizuri na imara kabla ya kupelekwa shambani lakini kwa sasa hali ya miche siyo nzuri na ina hali mbaya kutokana na ukosefu wa maji.

Amesema ili kunusuru hali hiyo, wanawaomba wadau wa zao hilo kuangalia namna ya kushughulikia tatizo hilo, huku akieleza uchimbaji mabwawa kuwa ndio msaada mkubwa kwa kuanzia.

Ameyashukuru makampuni ya ununuzi wa tumbaku ya Alliance One na JTI kwa kuanza kuchimba mabwawa kwa ajili ya maji au kupeleka maji kwa wakulima kwa kutumia magari.

Amebainisha kuwa kama hali ya ukame itaendelea, hata malengo ya kufikia kilo 100 milioni yatakuwa shakani na ndio maana wanapambana kunusuru hali hiyo.

Katika kunusuru miche hiyo, wakulima wanatumia maji yasiyo salama kumwagilia, wakilalamika ukosefu wa maji huku madimbwi yakitoa maji kwa shida.

Mkulima Hassan Kabanza ameeleza kuwa wanatumia maji yenye tope kumwagilia miche kutokana na ukame uliopo kwa sasa kwenye kijiji chao cha Igoko na maeneo yanayolima tumbaku.

Haya hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku, Stan Mnozya ameonya dhidi ya maji yenye tope kuwa yanazipa hewa na kuhatarisha uhai wa miche na kutaka maji ya tope yachujwe kutenganisha tope ili zisizibe hewa dhidi ya miche na ardhi.

Watumishi wa Bodi ya Tumbaku wanatembelea vitalu kuona namna vilivyo ili kusaidia miche ikue katika hali inayotakiwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live