Mwaka 1944 wakati vita vya pili vya dunia vikiendelea, Dola ya Marekani kwa mara ya kwanza ilitambuliwa kama sarafu iliyotunzwa na nchi nyingi kama akiba ya fedha za kigeni, kuanzia hapo imetawala biashara za kimataifa na shughuli za kifedha.
Mpaka Desemba, 2022 jumla ya dola za Kimarekani zilikuwa ni asilimia 58.9 ya fedha zote za kigeni zilizohifadhiwa katika benki kuu za nchi mbalimbali, mataifa yenye nguvu kubwa ya kiuchumi yakiongoza kuwa na kiwango kikubwa.
Sarafu ya Ulaya (Euro) inashika nafasi ya pili kama sarafu iliyohifadhiwa zaidi katika nchi mbalimbali kwa asilimia 20.47, ya tatu ni Paundi ya Uingereza asilimia 5.51, Yen ya Japan asilimia 4.59, Yuan ya China asilimia 2.69 na dola ya Canada kwa asilimia 2.36.
Hadi mwishoni mwa 2022 jumla ya fedha za kigeni zilizokuwa zimehifadhiwa katika benki kuu zote zilikuwa na thamani ya Dola za Kimarekani trilioni 11.96, kati ya hizo, dola za Kimarekani ni trilioni 6.47, euro 2.27 trilioni, zilizobakia ni chini ya trilioni moja.
Utawala wa dola katika miamala, biashara za kimataifa na shughuli za kifedha umeanza kutikiswa katika miaka ya hivi karibuni kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na nchi tofauti. Takwimu za IMF zinaonyesha kuwa mwaka 1999 Dola ya Kimarekani ilikuwa ni asilimia 71 ya fedha zote za kigeni zilizowekwa kama akiba.
Pengine kupungua kwa kiwango hicho kunatokana na hatua za baadhi ya mataifa mbalimbali kuongeza matumizi ya sarafu za ndani katika biashara za kimataifa sanjari na kupunguza matumizi ya dola na Euro kwa miamala ya kibiashara nje ya mipaka yao.
China, ambayo akiba ya fedha zake za kigeni inafikia Dola trilioni 3, Waziri wake wa mambo ya nje, Qin Gang, Februari mwaka huu, aliwaambia waandishi wa habari kuwa China na rafiki yake, Russia katika biashara zao watatumia sarafu yoyote yenye tija, salama na ya kuaminika: “sarafu haipaswi kuwa turufu ya vikwazo na uonevu kwa wengine”.
Katika kupunguza utawala wa dola ya Marekani kwenye miamala, mataifa zaidi ya 20 yameingia makubaliano yanayowapa uhuru wa kufanya biashara kwa kutumia sarafu zao wenyewe na mipango inaendelea kwa nchi nyingine.
China, India na Russia ndiyo nchi vinara zinazofanya mipango na kampeni za kutumia sarafu za ndani katika ufanyaji wa biashara na mataifa mengine.
Hadi kufikia mwezi Machi, 2023 Benki Kuu ya India (RBI) iliidhinisha benki kuu kutoka nchi 18 zikiwemo Tanzania, Kenya na Uganda kufungua akaunti maalum ya Vostro Rupee (SVRAs) ambayo itaziwezesha kulipa malipo ya Rupia za India kama hatua kubwa ya kupunguza utegemezi wa fedha za kigeni.
Takwimu za Biashara na Uwekezaji ya Afrika Mashariki ya 2020 zinaonyesha kuwa mauzo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwenda India yalikuwa Dola za Kimarekani 978.6 milioni, sawa na Sh2.3 trilioni na yale ya China dola 422.6 milioni (Sh990 bilioni).
Mchakato wa SVRA wa India ulianza mwaka wa 2022, baada ya RBI kutangaza kuwa imeamua kuweka utaratibu wa ziada wa ankara, malipo na ulipaji wa mauzo ya nje. Baadhi ya mataifa, ikiwemo Russia tayari yanafanya biashara na India kwa sarafu zao za ndani, nchi nyingine zilizoidhinishwa na RBI kufungua SVRA ni pamoja na Botswana, Fiji, Ujerumani, Guyana, Israel, Malaysia, Mauritius, Myanmar, New Zealand, Oman, Seychelles, Singapore, Sri Lanka na Uingereza.
Hatua za kupunguza matumizi ya dola na fedha za kigeni katika mataifa mbalimbali hazijaanza hivi karibuni, mwaka 2011 China na Japan zilikubaliana kuacha kutumia dola katika biashara zao na badala yake kutumia sarafu za nchi husika.
Mwaka 2013 China na Brazil zilikubaliana kuacha kutumia dola katika biashara zake, makubaliano yaliyofuata yalikuwa ni ya China na Saudi Arabia na sasa umekuwa ni mtindo mpya kwa nchi nyingi.
Kudorora kwa uhusiano kati ya Marekani na mataifa mengine pengine ni miongoni mwa mambo yaliyochochea kuongezeka kwa harakati za kupunguza matumizi ya sarafu hiyo, kwani baadhi ya mataifa yameumizwa na hatua zilichokuliwa na tarifa hilo la kwanza kwa uchumi duniani.
Akizungumzia hatua zinazochukuliwa na nchi yake katika kupunguza matumizi ya fedha za kigeni katika biashara, Balozi wa India nchini, Binaya Pradhan alisema kuanzia mwaka huu mpango uliopo ni kutoingiza fedha yoyote ya kigeni katika kufanya biashara kati ya Tanzania na India.
“Mazungumzo na Serikali yalishaanza na mwezi ujao ubalozi utakutana na mabenki ya hapa nchini kuzungumza kuhusu hilo, tunataka tuanze utaratibu huo mwaka huu wa 2023,” alisema Balozi Pradhan.
Akielezea faida za utaratibu wa kutumia sarafu za ndani, alisema suala la wabia wa kibiashara kutaka kutumia sarafu yao ni mtindo mpya wenye lengo la kuepuka kulipa gharama za miamala na kununua fedha za kigeni.
Alisema hivi sasa wafanyabiashara hulazimika kutumia sarafu yao kununua dola kisha dola ndio inunue rupee, lakini kitendo cha kununua fedha za kigeni ndiyo uweze kufanya manunuzi kinaongeza gharama za bidhaa, na kinadhoofisha sarafu ya ndani.
Mchambuzi wa Uchumi mwandamizi, Dk Abel Kinyondo alisema hatua ya nchi kupunguza matumizi ya fedha za kigeni katika manunuzi ya nje hutasaidia pia kupunguza mfumuko wa bei unaotoka nchi za nje kwa kuwa hatua ya kutumia sarafu ya ndani inapunguza gharama ya miamala.
“Utaratibu wa kutumia fedha za kigeni kwa manunuzi unapunguza akiba ya fedha za kigeni ambazo Serikali inazihitaji kwa kiwango kikubwa, lakini pia mahitaji ya fedha za kigeni yanapokuwa makubwa yanaongeza msukumo wa kushuka kwa sarafu ya ndani, hivyo hatua hiyo ni nzuri,” alisema.
Kuhusu juhudi za kupunguza utegemezi wa dola, Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar na Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja anasema kila Taifa lina maamuzi ya namna linavyotaka kufanya biashara, hivyo kama baadhi ya mataifa yameamua kuja na mipango ya kutumia fedha zao za ndani katika kutekeleza biashara zao ni jambo zuri.
“Haya ni maendeleo katika dunia, hakuna mtu wala taifa lolote duniani linataka kubaki nyuma,” anasema na kuongeza kuwa hakuna tafsiri yoyote mbaya kwa nchi kutumia sarafu nyingine katika masuala ya kibiashara, kwani kila taifa linakuwa na maamuzi sarafu gani nafuu kwa matumizi ya biashara zake.
Mchambuzi wa Uchumi, Humphrey Mosha yeye anasema nchi nyingi sasa zimeshatambua hakuna ulazima wa kutegemea Dola katika biashara za kimataifa, kwa kuwa thamani yake ipo juu, hivyo wanakuja na njia mbadala za kutumia sarafu zao.
“Ni jambo zuri kwa baadhi ya nchi kuanza kuhamasisha matumizi ya fedha zao za ndani katika biashara, jambo hili litasaidia baadhi ya mataifa kupunguza kutegemea dola kama sarafu muhimu katika biashara za kimataifa,” anasema Mosha.
Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Mwinuka Lutengano anasema kwa kutumia sarafu za ndani katika biashara kunaongeza mvuto kibishara, hivyo nchi zinazochagua kufanya hivyo zitanufaika.
“Jambo hilo litaleta mvuto katika biashara kwa kuwa baadhi ya nchi zitakuwa na maamuzi ni taifa gani afanye nalo biashara ili waweze kuwalipa kwa kutumia sarafu zao ambazo zinaonekana zitapunguza gharama,” anasema.
Anaongeza kuwa kutokana na baadhi ya nchi kuanza kutumia sarafu zao katika biashara za kimataifa, itawasaidia lakini itachukua muda kupunguza matumizi ya dola katika biashara mbalimbali za kimataifa.
“Matumizi ya dola yataendelea kuwepo kwa sababu kuna baadhi ya mambo hayatafanyika bila kutumia dola”