Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vita vya bajaji, teksi na daladala hapatoshi

Vita Picccc Bajaji Ndala Dala Vita vya bajaji, teksi na daladala hapatoshi

Tue, 25 Oct 2022 Chanzo: mwanachidigital

Ni mtifuano, hivi ndivyo unaweza kuelezea mvutano uliopo maeneo mengi katika miji mikubwa, kati ya pikipiki za miguu mitatu ‘bajaji’ kwa upande mmoja na magari ya abiria -- daladala na teksi -- kwa upande wa pili.

Pamoja na fursa za ajira na urahisi wa usafiri mijini ulioletwa na bajaji, katika baadhi ya miji zimegeuka kero kwa watumiaji wa barabara kutokana na wingi wake hizo ambao haulingani na miundombinu ya barabara iliyopo.

Kundi la bajaji ndilo linatajwa kukithiri kwa uvunjifu wa sheria za barabarani kwa sasa, ikielezwa kuwepo madereva wasiokuwa na leseni na kufanya kazi kinyume na leseni zao -- kujiendesha kama daladala badala ya kuwa usafiri wa kukodi na kutumika katika uhalifu.

Uchunguzi umebaini kutokana na ulegevu katika usimamizi wa sheria, kumekuwepo na misuguano kati ya madereva wa daladala na bajaji katika majiji ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Aidha, mivutano ya kila mara baina ya bajaji na daladala husababisha migomo na kusababisha adha kwa wananchi wanaohitaji kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine.

Kulingana na uchunguzi huo, kiini cha misuguano hiyo ambayo hufikia hatua ya madereva kupigana makonde, ni bajaji kujiendesha kinyume na masharti ya leseni zao na kupakia abiria katika vituo vilivyotengwa kwa ajili ya teksi na daladala.

Ingawa Mamlaka ya Udhibiri wa Usafiri wa Ardhini (Latra) ndio yenye wajibu wa kutoa leseni za bajaji, jukumu hilo limekasimiwa kwa halmashauri za majiji na miji kupitia maofisa biashara.

Lawama ni lazima

Latra imesema halmashauri haziwezi kuepuka lawama kwa kuwa hutoa leseni na kupanga maeneo yapi bajaji ziegeshwe.

Mkurugenzi wa Latra, Habib Suluo alisema tangu mamlaka yake ibadilishwe kutoka (Sumatra), iliachiwa jukumu la kusimamia Teksi na daladala pekee huku bajaji zikisimamiwa na halmashauri

Hata hivyo, Suluo alisema suala hilo halipo vizuri katika ufanyaji kazi na hivyo anatamani lirudi mikononi mwa mamlaka yake au lisimamiwe na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (Tarura) ambayo kwa muda mfupi wa kusimamia maegesho imeonyesha mafanikio makubwa.

“Jingine, pia halmashauri hazijawekea mkazo usimamizi na uendeshaji wa biashara ya bajaji na huko wangeweza kuvuna mapato mengi,” alisema mkurugenzi huyo.

“Ni kutokana na hilo kumekuwepo na watu wanaoendesha vyombo hovyo bila leseni ambao ni wengi lakini husikii hata kweye vikao vya mabaraza ya madiwani vikiongelewa na kuwekewa mkakati,” alisema Suluo.

Alipoulizwa kuhusu hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), David Silinde alisema halifahamu hivyo asingependa kuzungumzia jambo ambalo hana taarifa sahihi, bali anaomba muda alifuatilie.

Hali ilivyo Moshi

Mgongano wa vyombo hivyo uko dhahiri katika mji wa Moshi unaoelezwa kuwa na bajaji zaidi ya 4,000 wakati mahitaji kulingana uwezo wa njia zote ni bajaji 900, lakini barabara ya kwenda hospitali ya KCMC ambayo ni finyu ina Bajaji zaidi ya 900 peke yake.

Uchunguzi wa gazeti hili uliothibitishwa na viongozi wa bajaji, unaonyesha wingi wa bajaji katika baadhi ya njia --mfano KCMC na Mbuyu--- umekuwa ni kero, na wakazi wanazinyooshea kidole halmashauri.

Njia ya ya KCMC iliyotakiwa kuwa na bajaji kama 200, inakadiriwa kuwa zaidi ya 900, zikiwa chanzo cha ajali nyingi.

Mwenyekiti wa waendesha bajaji Manispaa ya Moshi, Hamad Bendera alisema Latra na Manispaa walivuruga utaratibu uliokuwepo awali kwa kuharibu kanzi data na kuwa chanzo cha kila mtu kuingiza bajaji katikati ya mji kiholela.

“Tulikuwa na utaratibu mzuri sana wakati wa mama Mghwira (marehemu Anna Mghwira-aliyekuwa RC Kilimanjaro) na tulikuwa na kanzi data ya ukomo wa kila njia, namba za ubavuni za kila bajaji, bima na kila kitu,” alisema Bendera.

“Lakini huo utaratibu ulivurugwa na leseni sasa zinatolewa bila kuangalia ukomo wa kila njia na kuna wanaonunua bajaji leo na kuingiza barabarani kwa kujiandikia namba za ubavuni wenyewe. Imekuwa vurugu mtindo mmoja,” alisema.

Mwenyekiti wa madereva daladala Mkoa wa Kilimanjaro, Cathbert Temu alisema bajaji zimekuwa ni kero barabarani kutokana na kufanya kazi kama daladala, hali ambayo inafumbiwa macho na mamlaka zinazohusika kusimamia sheria.

“Hapa Manispaa ya Moshi daladala zaidi ya 300 zimeondolewa barabarani kutokana na hii changamoto ya utitiri wa bajaji. Daladala za Majengo, Soweto, KCMC na baadhi ya njia zimeondolewa barabarani,” alisema Temu.

Ofisa Mfawidhi wa Latra Mkoa wa Kilimanjaro, Paul Nyelo alisema bajaji zimesajiliwa kwa mujibu wa sheria lakini kinachofanyika ni ukiukwaji wa masharti ya leseni kwa kujiendesha kama daladala.

Kuhusu daladala zilizoondoka barabarani, aliwataka wale wote walioondoa magari yao barabarani kwa namna moja au nyingine wayarudishe ili waendelee kutoa huduma kwa wananchi.

“Tumewaambia wale wote walioondoa magari barabarani wayarejeshe katika zile njia zao na sisi tupo tayari kuwasajili tena, hili suala la mgogoro wa bajaji na daladala ni tatizo ambalo lipo kila mkoa na hii ni kutokana na miji kukua,” alisema.

Urahisi wa usafiri

Katika Jiji la Dar es Salaam, msuguano zaidi upo kati ya madereva bajaji na teksi kutokana na kuingiliana katika vituo huku wananchi wao wakifurahia ujio wa bajaji kuwa umerahisisha usafiri, hasa asubuhi na jioni.

Mustapha Mbawala, mwenyekiti wa madereva teksi Kivukoni-Feri alisema biashara hiyo imeharibika kwa asilimia 100 kutokana na ujio wa bajaji kwani awali kwa siku walikuwa wakipata abiria watano lakini sasa hata wawili ni kazi.

Pia alisema walikuwa wakiondoka na Sh80,000 hadi Sh100,000 kwa siku lakini sasa kupata Sh 30,000 ni kazi na wenye bajaji wamekuwa wakiwafanyia vurugu kwa kutafuta wateja badala ya kusibiri vituoni.

Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya waendesha Pikipiki na Bajaji, Said Chenja alisema wanaopinga uwepo wa bajaji mjini hawana uelewa kwani kila mtu anaruhusiwa kufanya biashara halali.

“Hao teksi kila wakati wanatulalamikia tumewaharibia biashara. Walitaka wafanye biashara peke yao? Mbona kuna tunaowajua wameshindwa biashara ya teksi wamekuja kwenye bajaji na sisi tuwafukuze?” alihoji Chenja.

Hata hivyo, Chenja alikiri baadhi ya madereva wa bajaji kugeuka kuwa kero mjini, hasa wale wanaoegesha vyombo vyao kwenye maeneo yasiyo rasmi.

Kwa upande wananchi, akiwemo Monica Shirima, mkazi wa Mbezi wamesema bajaji zimekuwa msaada kwao kutokana na usafiri kutoka mjini kwenda maeneo kuwa wa tabu.

Monica alisema baada ya magari ya mwendokasi, daladala Mbezi - Kariakoo na Posta ziliondolewa, lakioni hata hayo ya mwendokasi yanaonekana kuzidiwa asubuhi na jioni, hivyo bajaji zinakuwa mkombozi.

Elisha Egbert, mkazi wa Buza kwa Mpalange, alisema kwao hakuna kabisa daladala hivyo bajaji zimekuwa mkombozi kuwatoa zinapoishia daladala hadi nyumbani huku Nelson Mushi yeye anadai kajaji ni kero na zinasababisha foleni mijini.

Arusha, Dodoma, Mbeya pagumu

Wakati Latra mkoa Arusha, ikisitisha usajili mpya wa bajaji kufanya kazi za usafirishaji ndani ya jiji la Arusha, baadhi ya wananchi wamepinga uamuzi huo wakitaka vyombo vya usafiri vishindane kupata abiria kwa mujibu wa sheria.

Katika jiji hilo, kumeibuka mgogoro baina ya bajaji na daladala katika barabara za Unga Ltd, Sombetini, Sanawari na maeneo ya Daraja Mbili kufuatia wenye daladala kulalamikia wingi wa bajaji ambao unawakosesha abiria.

Ofisa Mfawidhi wa Latra mkoa wa Arusha, Amani Mwakalebela alisema wameamua kisitisha utoaji wa leseni kutokana na wingi wa bajaji zilizopo tofauti na hali halisi ya zilizosajiliwa kutoa huduma.

“Bajaji zilizosajiliwa hazizidi 1,000 lakini zinazofanya kazi ziko zaidi ya 3,000 na mbaya zaidi wanafanya kazi nje ya usajili wao,” alisema Mwakalebela.

Katibu wa chama cha wasafirishaji mkoa wa Arusha na Kilimanjaro (Akiboa), Locken Adolf alisema wao kama wasafirishaji hawapingi bajaji kutoa huduma lakini wanataka utaratibu ufuatwe juu leseni na usajili wao.

Kwa upande wake, mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani humo, Solomon Mwangamilo alisema kundi linalowaumiza kichwa Jeshi la Polisi ni madereva bajaji kutokana na ukaidi wao wa kufuata sheria.

Mwenyekiti wa mpito wa Umoja wa wenye Bajaji jiji la Arusha (Uwabaja), Joseph Mwita alisema changamoto kubwa ni usajili na vituo vya maegesho, hivyo wanaiiomba Serikali kuwaongezea muda wa kujisajili Latra ili kujiendesha kihalali.

Kama walivyoeleza katika maeneo mengine Dar, Moshi na Mbeya, baadhi ya wakazi wa Arusha wamesema bajaji zimeleta unafuu kwa kuwa awali kulikuwa na msongamano wa abiria na foleni na sasa vimepungua.

Hata hivyo, Neema Lukumay mkazi wa Kwamrombo alisema Latra inapaswa kuachia soko huria biashara ya usafiri, nao kama mamlaka wajikite kutoa leseni kwa kuzingatia barabara lakini si kuzuia usafiri huo.

Jijini Mbeya, Katibu wa Umoja wa Madereva Bajaji na Wamiliki (Umabamimbe), Lucas Mwakyusa alisema kwa sasa hakuna msuguano baina yao na daladala baada ya viongozi kukaa na kuweka ramani ya maeneo ambayo bajaji zinaishia.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa madereva wa daladala Kanda ya Mbarizi, Ulimboka Mwambai alisema bado tatizo la mwingiliano lipo licha ya kugawana njia, kwa kuwa bajaji zinaendelea kukiuka utaratibu uliowekwa.

Jiji la Dodoma halijanusurika na misuguano pia baina ya daladala na bajaji lakini Latra imesema leseni ya bajaji zinawataka kubeba abiria katika vituo walivyopangiwa kwenda na kurudi na si kupita katika vituo vya daladala.

“Kumekuwa na hiyo shida kwamba bajaji inapeleka abiria eneo fulani na wakati wa kurudi wanapakia abiria njiani,” alisema ofisa wa Latra, Ezekiel Emmanuel.

Dereva wa bajaji eneo la Kikuyu, Aminius Mwaimu alikiri yeye binafsi kuingia kwenye mgogoro mara kwa mara na daladala kwa kugombea abiria, akisema hivi karibuni mmoja wao (bajaji) lichomwa kisu na mwenzie wakigombea abiria.

Bajaji zipakwe rangi ya njia

Sababu za migogoro katikamiji hiyo mikubwa hazitofuatiani na za Jiji la Mwanza ambako Hussein Mosha, mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Chama cha Madereva na Makondakta wa Daladala (Mwareda), alisema mgogoro kati yao unasababishwa na bajaji kubeba abiria kama daladala, tena kwa bei ya daladala.

“Siyo tu wameingilia njia za kawaida za daladala, bali pia wenye bajaji sasa wanaokota abiria mmoja mmoja sawasawa na tunavyofanya sisi daladala kinyume cha usajili wao wa kufanya kazi kwa kukodishwa,” alisema.

“Katika njia zote hizo bajaji wanapakia abiria kwa nauli ya Sh500 ambayo pia ndio inatozwa na daladala; kama imeshindikana kuzuiwa, basi bajaji zisajiliwe na kupakwa rangi kuonyesha njia zinazopaswa kupita kama daladala,” alisema Mosha.

Wakati mwenzake wa daladala akilalamika, Elias Lugwisha, mwenyekiti wa madereva wa bajaji Mkoa wa Mwanza, alisema kinacholeta mgogoro ni masilahi kutokana na abiria wengi kupenda bajaji kuliko daladala kwa sababu licha ya kupakia watu wachache, pia haisimami kila kituo baada ya kupakia.

“Penye kipato lazima kuna mgogoro wa kimasilahi. Abiria wengi, hasa wenye haraka hupendelea usafiri wa bajaji kwa sababu tunapakia abiria wachache na hatusimami njiani kama daladala. Hii inapunguza kipato cha wenye daladala. Huo ndio mgogoro kati yetu. Mengine ni visingizio tu,” alisema Lugwisha.

Akizungumzia mvutano kati ya makundi hayo, Ofisa Mfawidhi wa Latra Mkoa wa Mwanza, Halima Lutavi alisema unafuu wa gharama na uharaka wa safari kwa bajaji ndiyo kiini cha mvutano uliopo.

Hata hivyo, abiria wanataka suala la usafiri liachwe liwe huru ambapo Hawa Abdallah, mkazi wa Kanyerere alisema “hakuna mtu anayelazimishwa kupanda daladala, bajaji, pikipiki wala teksi; kila abiria anachagua aina ya usafiri wa kutumia kwa kuzingatia uwezo wake, mahitaji na muda.”

Chanzo: mwanachidigital