Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana juu ya mpango wa kuzuia zaidi ya theluthi mbili ya uagizaji wa mafuta kutoka Urusi.
Marufuku hiyo ni maelewano ambayo hayataathiri uagizaji wa mafuta ya bomba kwa sasa, kufuatia upinzani kutoka Hungary.
Mkuu wa Baraza la Ulaya Charles Michel alisema makubaliano hayo yalikata “chanzo kikubwa cha ufadhili” kwa mashine ya vita ya Urusi.
Ni sehemu ya kifurushi cha sita cha vikwazo vilivyoidhinishwa katika mkutano wa kilele mjini Brussels, ambapo nchi zote 27 wanachama zimelazimika kukubaliana.
Bw Michel alisema EU pia imekubali hatua kali zinazolenga benki kubwa zaidi ya Urusi, Sberbank, na mashirika matatu ya utangazaji yanayomilikiwa na serikali.
Wanachama wa Umoja wa Ulaya walitumia masaa mengi kuhangaika kusuluhisha tofauti zao kuhusu marufuku ya uagizaji mafuta ya Urusi, huku Hungary ikiwa ni mpinzani wake mkuu.
Maelewano hayo yalifuatia mabishano ya wiki kadhaa hadi ikakubaliwa kuwa kutakuwa na “msamaha wa muda kwa mafuta unaokuja kwa njia ya bomba kwenda kwa EU”, Bw Michel aliwaambia waandishi wa habari.