Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi, wadau waja na maazimio zao la kahawa Mbozi

Kahawa Pc Viongozi, wadau waja na maazimio zao la kahawa Mbozi

Fri, 16 Jun 2023 Chanzo: mwanachidigital

Wadau wa kahawa na viongozi mbalimbali wilaya ya Mbozi mkoa wa Songwe wamefikia maazimio ambayo yatasaidia kuwainua wakulima wa zao hilo katika wilaya hiyo.

Maamuzi hayo yamefikiwa leo Jumatano Juni 14, 2023 wakati wa mafunzo ya viongozi na wadau wa kahawa Wilaya ya Mbozi ya kuwajengea uelewa wa pamoja juu ya mnyororo wa thamani wa zao la kahawa.

Miongoni mwa maazimio hayo ni pamoja na kuitaka ofisi ya kilimo isaidie kuzunguka na kukagua uhifadhi wa zao la kahawa kwenye stoo za wananchi ili kubaini hali ya utunzaji.

Pia, wameazimia kuwa vyombo vya dola kufanya ukaguzi katika vyamba vya ushirika na vikibaini ubadhirifu hatua zichukuliwe mapema.

Azimio lingine ambalo wadau hao wamefikia ni ukaguzi wa mizani wa mara kwa mara ili kuepusha wizi unaotokana na mizani zisizo na viwango.

Katika mafunzo hayo wadau hao na viongozi wametaka mikataba iwe ya wazi ambayo itawashirikisha wakulima wa zao hilo ili kuepuka mikataba kandamizi.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Songwe, Edings Mwakambonja amewataka viongozi hao na wadau kusimamia vyama vya ushirika vya wakulima (AMCOS) ili kudhibiti ubadhirifu unaoweza kujiyokeza.

"Katika dhana ya utawala bora lazima tuzingatie uwazi na ushirikishwaji. Bila vitu hivyo dhana ya utawala bora inapotea" amesema na kuongeza;

"Ipo mianya mingi ya rushwa katika AMCOS ikiwa ni katika mchakato wa upatikanaji wa viongozi, ukopaji, makato mbalimbali na matumizi mabaya ya mali za AMCOS" amesisitiza

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Samson Nzunda amewataka maafisa ushirika kuwapa elimu mara kwa mara viongozi wa AMCOS ili kufanya kazi kwa ufanisi.

Pia, ametoa rai kwa madiwani na viongozi wa ushirika kushirikiana kwa kupeana taarifa ili kuwa na taarifa ya kile kinachoendelea huku akiwataka madiwani kutumia nafasi zao kuwapa elimu wakulima.

Naye Mkurugenzi wa Masoko na Ubora wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Frank Nyarusi amewataka madiwani kuweka mikakati ya uzalishaji wa kahawa katika wilaya hiyo kwani bidhaa hiyo inahitajika kwa wingi.

"Kahawa ya Tanzania ni chumvi ya kahawa zingine duniani hasa kahawa kutoka Mbozi" ameeleza

Amewaasa viongozi wa vyama vya ushirika kufanya utafiti wa bei za kahawa kabla ya kusaini mikataba na wanunuzi ili kuepusha migogoro.

Awali akizungumza katika mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi (DC), Esther Mahawe ametaja faida za mafunzo hayo kuwa ni pamoja na kutatua changamoto za kukosa uelewa wa pamoja juu ya taratibu za kitaalamu, kiufundi na kifedha katika mnyororo wa thamani kama vile uzalishaji na uongezaji wa thamani wa zao la kahawa, usimamizi wa vyama vya ushirika, mikataba ya wadau, mfumo wa masoko na utaratibu wa ukusanyaji ushuru wa halmashauri.

Amewataka viongozi kutoa elimu kwa akina mama na vijana kuendeleza zao la kahawa kutokana na taswira ya sasa ambayo inaonyesha kuwa zao hilo ni la kinababa.

Mafunzo hayo yamewahusisha wajumbe Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Mbozi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Madiwani, maafisa ushirika na wadau wa kahawa kutoka wilaya hiyo.

Chanzo: mwanachidigital