Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, amewataka Viongozi wa Vyama Vikuu vya Ushirika (UNION) kuwa wabunifu katika kuwahuduma wakulima na kuacha kusubiri biashara ya minada.
Dkt. Ndiege amesema kuwa Maafisa masoko wa UNION wawezeshwe wakatafute masoko ya mazao ndani ya nchi na nje ya nchi na kuacha kusubiri wanunuzi kuja katika maeneo yao na bei zao.
Amesema hayo leo wakati akifanya ziara ya kikazi aliyoambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi za Ghala katika Vyama Vikuu vya TANECU, RUNALI NA MAMCU katika Mikoa ya Mtwara na Lindi.
Dkt Ndiege amesema kuna haja kwa viongozi kuanza kutafuta masoko wenyewe kabla ya msimu haujaanza, au kuangalia namna ya wao kuwa wanunuzi wa mazao hayo kwa bei ambayo itamnufaisha mkulima.
“Jipambanueni na jiongezeni, nyie mnafanya kazi kwa maslahi ya wakulima anzeni biashara ya ununuzi wa mazao yanayouzwa kipindi cha msimu alafu nyie mtauza baada ya msimu kuisha. Wahudumieni wakulima wenu kwa kulinda maslahi yao,” amesema Dkt Ndiege.
Dkt Ndiege amewataka viongozi hao kuacha kutegemea misimu miwili tu ya Korosho na Ufuta na waanze kufikiria kuingiza mazao mengine katika mfumo wa Stakabadhi Ghalani na pia watafute mazao mengine ambayo wakulima watalima na wataingiza kwenye mfumo wa Stakabadhi Ghalani.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, Asangye Bangu, amekemea kitendo cha waendesha maghala ambao wana tabia ya kukatia mzigo stakabadhi kabla haujafika ghalani.
“Fuateni sheria acheni kuvunja utaratibu, subiri mzigo ukufikie ghalani kwako ndiyo utoe Stakabadhi kwa wenye mizigo na nyie viongozi wa AMCOS ambao mnashirikiana na waendesha maghala kufanya hivi acheni hizo tabia,” amesema Bangu.
Bwana Bangu amesisitiza kuwa akibainika Mwendesha ghala anayefanya hivyo atachukiliwa hatua, kama kanuni na taratibu za uendesha ghala zinavyoelekeza.
Aidha, amevishauri vyama vya AMCOS kufungua kampuni za ubanguaji tkorosho ambazo wanaweza kuanza kidogo kidogo na jambo hili litasaidia kulinda masilahi ya wakulima wao pale ambapo kunakuwa na hali ya kushuka kwa bei wao watanunua kwa bei yenye kumnufaisha mkulima.