Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vilio Kariakoo

Bd79d95b4140e9b816f885065c168c1b.png Vilio Kariakoo

Mon, 12 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Ummy Mwalimu amesema taarifa za awali zinaonesha mato uliounguza soko kuu la Kariakoo umeathiri wafanyabiashara 224.

Ummy aliandika kwenye ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter kuwa wanasubiri taarifa ya uchunguzi ya tume aliyoiunda Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

“Taarifa zetu za awali ni kuwa wafanyabiashara 224 ni wahanga (waathirika) wa janga hili. Pia tumepokea taarifa kuna wengine mali zao zimepotea/ kuibiwa”aliandika jana jioni.

Katika ukurasa rasmi wa Tamisemi,Ummy alieleza kuwa moto katika soko hilo umetoa fundisho na kuanzia sasa masoko yote makubwa yanayomilikiwa na halmashauri na stendi kubwa ikiwemo ya Magufuli iliyopo Mbezi, Dar es Salaam zitawekwa vifaa vya kuzimia moto na visima vya maji ili kukabiliana na majanga ya moto.

“Masoko yote yanayomilikiwa na Halmashauri zetu, hususani masoko makubwa, stendi zetu zote ambazo zinamilikiwa na Halmashauri zetu tutahakikisha zinakuwa na visima vya maji, ili kuweza kukabiliana na majanga haya ya moto.”aliandika kwenye ukurasa huo.

Awali jana Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga alisema walifanifanikiwa kuudhibiti moto kwa asilimia 100 lakini changamoto ilikuwa ni umbali wa kuchukua maji.

“Ilichukia muda mrefu kwa sababu moto ulikuwa mkubwa hapa Kariakoo hamna sehemu za maji tulikuwa tunafuata maji mbali ilifanya kazi kuwa ngumu”alisema na kuongeza;

“Bado hakuna shughuli yoyote inayoweza kufanyika hapa kwa sababu moshi unafuka , tunafanya uchunguzi kubaini chanzo cha moto ,hakuna majeruhi wala vifo.

Waziri Mkuu

Jana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa siku saba za awali kwa tume aliyoiunda kuchunguza chanzo cha moto katika soko hilo, Dar es Salaam.

Alisema kamati iliyoundwa itafanya kazi na kamati ya ulinzi na usalama iliyoanza kufanya kazi chini ya Mkuu wa Mkoa wa

Dar es Salaam na itajumuisha Ofisi ya Rais-Ikulu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, na Ofisi ya Waziri Mkuu itakayowakilishwa na Mkurugenzi wa Maafa.

Wengine ni vyombo vya ulinzi na usalama vikujumuisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Zimamoto na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Majaliwa alisema kamati hiyo pia itajumuisha Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Majaliwa aliwapa pole waathirika wote na kusema kuwa kamati iliyoundwa itatumia siku saba kuchunguza.

“Rais Samia alipata taarifa ya moto na kuja kunipa maelekezo ya kuja kuona hali halisi ya bidhaa zilizoungua ambazo ndizo zinaipa hadhi eneo hili la Kariakoo na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango anatoa pole”alisema na kuongeza;

Majaliwa alisema, pamoja na mambo mengine kamati hiyo itaainisha mali zilizopotea au kuungua na kujua tathimini ya jengo hilo.

“Tunataka kujua

jengo baada ya moto nini kifanyike? Kwa sababu mara nyingi kunapokuwa na moto kuta zinakuwa teketeke jengo hili ni imara na wataalamu watatushauri na serikali haitasita kama watasema tujenge lingine tutajenga kwa ajili ya kurejesha wafanyabiashara.

Majaliwa alisema endapo itabainika kuna watu walifanya tukio hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Tunatambua mheshimiwa Rais alipotembelea hapa aliunda tume ya kufanya mapitio mbalimbali dhidi ya tuhuma mlizosema nyie wenyewe inawezekana sijui labda tume hiyo ilianza kubaini kitu kama kuna uhusiano na wale waliobainika na tume hatua kali itachukuliwa kwahiyo taarifa ya ile tume itaingia kwenye hii nyingine”alisema na kuongeza;

“Kitendo cha kungua soko la miaka mingi lazima kuwe na uchunguzi wa kina hizo ni hatua ambazo tunachukua muwe watulivu,kwa sasa eneo hili sio salama kwenu,”

Majaliwa alisema vyombo vya ulinzi na usalama na zimamoto vitandelea na ulinzi katika eneo hilo na kuwataka wananchi wawe watulivu.

“Zima moto imeelekeza kuwa moto bado ni hatarishi hatujajua kama bado kuna maeneo ya mlipuko kama mitungi ya gesi na nyaya za umeme,mitambo inayouzwa bado sio salama na

tumeelekeza vyombo vyetu vya ulinzi kulinda usalama na pia kuhakikisha moto hauendelei tena na watakua hapa mpaka patakapotulia.

“Nawasihi wananchi kuwa watulivu kwasababu serikali iko hapa mpaka

tutakapojua ni nini chanzo chama moto, tunajua tukio kama hili likitokea kunakuwa na maeneo mengi sana nawasihi mtulie.

“Tunachoshukuru kule chini hakuna moto na mali zote zinalindwa ziko salama , soko dogo nalo liko salama na ulinzi mkali upo,”alisema.

Alisema serikali itaangalia namna ya kuwasaidia wafanyabiashara waliokopa

benki ikiwa ni pamoja na kuzungumza na benki hizo.

“Tume ile itapata taarifa zote kwa wenye mikopo rasmi ya taasisi za ukopeshaji kuongeza muda ili hata waje kulipe badae kutakapo tulia ,tutazungumza lugha moja na benki na watatuelewa ,”alisema.

Samia atoa agizo

Jana Rais Samia Suluhu Hassan aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama vichunguze ili kufahamu chanzo cha moto katika soko hilo.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Jaffar Haniu jana katika taarifa yake alieleza kuwa Rais Samia pia alitoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla na wafanyabiashara katika soko hilo.

Aliwapa pole kutokana na hasara waliyoipata kutokana na kuungua moto kwa soko hilo jijini Dar es Salaam.

Taarifa hiyo kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa Rais Samia alisema Soko Kuu la Kariakoo ni kubwa na lina mkusanyiko mkubwa wa wafanyabiashara.

Kwa mujibu wa Haniu Rais alisema kuteketea kwa soko hilo kutakuwa kumesababisha hasara kubwa kwa wapangaji na wamiliki wa soko hilo kongwe nchini.

Rais Samia alisema Soko la Kariakoo licha ya kuajiri wafanyabiashara wengi lakini ni kitovu cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki hivyo tukio hilo si hasara

kwa wafanyabiashara tu bali hata kwa serikali.

Soko la Kariakoo linasimamiwa na Shirika la masoko Kariakoo lilianzishwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge Na.36 ya mwaka 1974.

Historia ya soko

Uamuzi wakujenga soko kuu la Kariakoo la sasa ulifanywa na serikali mwaka 1970 na kuiagiza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kufanya mipango ya ujenzi wa soko jipya la kisasa ambalo lingechukua nafasi ya soko la zamani lililokua hapo Kariakoo.

Moto Morogoro

Wakati huohuo, Rais Samia jana alitoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martin Shigella na Jumuiya za Kiislaam Tanzania kufuatia kuungua moto kwa bweni la Shule ya Sekondari ya Kiislam ya Wasichana AT TOWN inayomilikiwa na Taasisi ya Kiislam iliyopo mji Mpya katika Manispaa ya Morogoro.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana kiliungana na Mwenyekiti wa chama hicho Rais Samia kutoa pole kwa waathirika wa moto katika soko la Kariakoo na kwenye shule ya wasichana ya Kiislamu ya At-Taaun mkoani Morogoro.

“Ni imani yetu serikali iko makini sana kufuatilia kadhia hizo na hatua stahiki zitachukuliwa”ilieleza taarifa ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka.

Chanzo: www.habarileo.co.tz