Timu ya maafisa wa Kenya na Tanzania wameweka mkakati wa kuondoa vikwazo vya ushuru ifikapo desemba mwaka huu ambavyo vimekuwa vikiathiri biashara miongoni mwa mataifa hayo mawili.
Hatua hiyo imekuja kufuatia mkutano wa pamoja wa Tume ya Ushirikiano (JCC) ambayo iliundwa kwaajili ya kutatua matatizo na vikwazo vilivyopo ambavyo vinaathiri maeneo yote ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Mkutano huo uliofanyika kwa muda wa siku tano jijini Nairobi ulimalizika siku ya jumanne nakukubaliana kuondoa vikwazo vya kudumu ambavyo vinaathiri biashara hasa katika biashara zinazofanyika mipakani.
"Katika biashara JCC imezingatia yale yaliyobainishwa na kamati ya biashara ya pamoja kutatua changamoto 30 kati ya 64 ambazo zinakabili uhusiano wa nchi hizo mbili na changamoto 34 zilizosalia zitatatuliwa mwishoni mwa mwezi desemba 2021". mmoja wa washiriki wa mkutano huo amesema.
Miongozi mwa changamoto 30 zilizotatuliwa ni pamoja na kuondoa ushuru kwenye vinywaji, kuondoa ada za ukaguzi wa bidhaa zilizosindikwa zenye alama za ubora.
Mwezi mmoja baada ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kufanya ziara Kenya, Kamati ya biashara ya pamoja ilibaini vizuizi 60 vilivyo na ushuru na visivyo na ushuru baina ya mataifa mawili.