Wafanyabiashara wadogo katika mpaka wa Tanzania na Kenya, eneo la Horohoro na Lungalunga ,wametaka serikali za Tanzania na Kenya, kuondoa vikwazo vya kibiashara ,hasa baada ya kukamilika miundombinu ikiwepo barabara ya Tanga- Horororo.
Barabara la lami ya Tanga- Horohoro, imejengwa na Serikali ya Marekani kupitia miradi ya malengo ya milenia (MCC).
Wakizungumza na mwandishi habari katika mpaka huo, baadhi ya wafanyabiashara wadogo wa Kenya na Tanzania, walitaka serikali za Kenya na Tanzania, kuendelea kupunguza vikwazo ili biashara iwe rahisi zaidi baina ya nchi moja hadi nyingine, hasa ya mazao, mifugo na bidhaa za ndani.
Joseph Mwanganya mfanyabishara mdogo wa Kenya kaunti ya Lungalunga, amesema licha ya serikali za Afrika mashariki kuwa na miundombinu bora mipakani lakini, bado changamoto kuwa ni vikwazo vya kibiashara.
“Sisi kama wafanyabiashara tunataka uhuru wa kufanya biashara hasa hizi ndogondogo turuhusiwe kuingia katika nchi hizi mipakani na kupitisha biashara ndogondogo hasa hizi za mazao,” amesema.