KAMPUNI ya Waandaaji wa maonesho ya Biashara, Kilimo, Uwekezaji na Utalii ya Afrika Mashariki (EAC EXPO), wameishukuru serikali mkoani Kagera juu ya kuondoa vikwazo mpakani na kusaidia wafanyabiashara wa Jumuia ya Afrika Mashariki kufika kwa wakati na kuleta bidhaa zao za ubunifu.
Maonesha hayo ambayo yanaandaliwa na SPACT CO LTD kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, amewakusanya wafanyabiashara zaidi ya 400 kutoka Tanzania ,Rwanda, Burundi na Jmahuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Wafanyabiashara hao wameleta biashara zao za ubunifu kwa ajili ya kutangaza masoko na kubadilishana uzoefu kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na nchi nyingine za Jumuia ya Afrika Mashariki.
Mratibu wa Maonesho yanayofanyika viwanja vya CCM Bukoba, Alden Kiraja amesema vikwazo kwa wafanyabiashara wanaokuja katika maonesho vimepungua na wengi wamefika kwa wakati, ukilinganisha na mwaka jana, ambapo wengi wao walikwama mpakani.
“Tunaendelea kuipongeza serikali kwa kushughulikia kero, hasa kwa mwaka huu, ambapo Mkuu wa Mkoa alishughulikia haraka barua ya utambuzi wa wafanyabiashara wanaotaka kushiriki maonesho ya EAC EXPO mkoani Kagera.
“Hii imetutia sana moyo na imewavutia wafanyabiashara wengi Kuja kushiriki, maonesho haya huchochea fursa za kibiashara na kufahamiana zaidi, kubadilishana ujuzi na kutangaza Mkoa wa Kagera kitalii na Tanzania kwa ujumla,” alisema Kiraja.
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonesho hayo Dk Abel Mahanga, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Muleba, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatuma Mwasa, alitoa wito kwa taasisi zinazotoa vibali kwa wafanyabiashara kupunguza urasimu wa kutoa vibali, kwani mfanyabiashara hapendi kupoteza muda.
Amesema ameridhishwa na bidhaa zilizoletwa na wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki baada ya kutembelea mabanda yao na kuwataka wakazi wa Kagera kutumia maonesho hayo kama sehemu ya kupata ujuzi na kuangazia fursa zilizoko katika nchi nyingine.
Alisema pia viongozi wa serikali na taasisi binafsi zitaendelea kushirikiana kuhakikisha changamoto za wafanyabiashara zinapungua na kuisha kabisa, huku akitoa wito kwa wadau wa maendeleo mkoani Kagera kuhakikisha wanaendelea kuwa wabunifu katika biashara zao, ili ubunifu huo ulete tija na kuwapatia masoko katika nchi zinazowazunguka. Maonesho hayo yatamalizika Julai 9, mwaka huu.