Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijiji 9,055 vitakuwa na umeme kufikia Julai 2020

51351 Pic+mgalu

Wed, 10 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewaondoa hofu wabunge kuhusu usambazaji wa umeme unaofanywa na Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) ambapo hadi kufikia Julai mwaka 2020 vijiji 9,055 vitakuwa na umeme.

Ameyasema hayo leo Aprili 9, 2019 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi  ya ofisi ya Waziri Mkuu na Mfuko wa Bunge mwaka 2019/2020

Amesema tangu julai Mosi, 2016 hadi 30 Machi mwaka huu vijiji 1,969 vilipata umeme na ukichanganya na vijiji ambavyo vilikuwa vimeshapatiwa umeme kabla ya Juni mwaka 2016 inakuwa jumla ya 6,365 kati ya vijiji 12,268.

Amesema hiyo ni sawa na asilimia 52 ya vijiji vyote kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Amesema hadi kukamilika kwa mradi huo ambao ni wa miezi 24, Juni 30 mwaka 2020, vijijini 9,055 vitakuwa na umeme nchini na vijiji vilivyobakia 3,213 ambavyo taratibu za kuvipatia umeme zimeshaanza kupitia mzunguko wa pili wa awamu ya tatu ya Wakala wa Umeme Vijijini (Rea).

“Naomba niwatoe hofu, tumetoa maelekezo kila wiki tuwashe takribani vijijini vitatu…Mtuamini kuwa uwezo tunao na nguvu tunayo ya kulisimamia hilo,” amesema.

Akizungumzia miradi mikubwa wanayoifanya amesema wanakuja na mradi wa ujazilizi ambao utagusa vitongoji ambapo zaidi ya Sh290 bilioni zimetengwa na Serikali.

Subira amesema uamuzi wa kisera umefanywa kuwa umeme utakaopelekwa vijijini kuwa na bei Sh27000  inayofanana bila kujali aliyeupeleka.

 “Serikali itaendelea kupambana na vishoka wanaoongeza bei kwa wananchi na hii italeta matumaini, tunawaambia waendelee kusubiri, ”amesema.

Aidha, amesema kuwa Serikali haijahama katika uchumi wa gesi na kwamba wanaendelea kuzalisha umeme na kuisambaza kwa watumiaji.



Chanzo: mwananchi.co.tz