Serikali imesema hadi kufikia mwezi Machi 2024 jumla ya vijiji 11,837 sawa na asilimia 96.37 ya vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vilikuwa vimeunganishiwa huduma ya umeme.
Hayo yamesema na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko Bungeni jijini Dodoma wakati akisoma hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Aidha, Dkt. Biteko amesema katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi vijijini, jumla ya taasisi 63,509 zinazotoa huduma kwa jamii ikiwemo ya elimu, biashara, pampu za maji, vituo vya afya na nyumba za Ibada zilikuwa zimeunganishiwa umeme ikilinganishwa na taasisi 43,925 za Aprili, 2023.
Vilevile, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kupeleka umeme vitongojini, katika visiwa na maeneo yaliyo mbali na Gridi ya Taifa, vituo vya afya na pampu za maji, wachimbaji wadogo wa madini, viwanda na kilimo, katika shule pamoja na mahakama za mwanzo vijijini.