Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana wapatiwa mkopo wa Sh319 mil

8846 Mkopo+pic TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Muleba. Halmashauri wilayani hapa Mkoa wa Kagera imetoa mkopo wa Sh319.2 milioni kwa vikundi 27 vya vijana, wanawake na walemavu kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali.

Ofisa Habari wa halmashauri hiyo, Lucy Binamungu alisema hayo juzi wakati wa mafunzo ya ujasiriamali kwa vikundi 30 vya walengwa katika robo tatu ya mwaka wa fedha 2017/18 ambavyo vimepokea Sh129.2 milioni.

Kati ya fedha hizo, vikundi vitatu vya kata za visiwani vimepatiwa mkopo wa Sh20.2 milioni.

Alisema katika mafunzo hayo, vikundi 18 vya vijana vimepata Sh187 milioni, saba vya wanawake vimepokea Sh132 milioni na viwili vya walemavu vimekopeshwa Sh4.6 milioni sawa na asilimia mbili kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na Serikali.

Fedha hizo alisema ni makusanyo kutoka mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2017/18.

“Tunatekeleza agizo la Serikali la kuhakikisha makundi hayo yanapata mikopo ya fedha na kuanzisha miradi ya kujiendeleza kiuchumi,” alisema Binamungu.

Alifafanua kuwa awali vikundi vya wanawake vilipata mkopo wa Sh187 milioni na vijana Sh132 milioni, kabla ya mabadiliko ya kuwa na mwongozo mpya wa kuhakikisha walemavu wanapata mkopo wa asilimia mbili ya mapato ya ndani.

Ofisa Biashara wilayani Muleba, Keneth Mariro aliwataka wajumbe wa vikundi hivyo kuanzisha miradi kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa ili kujikwamua na umaskini kwa kukuza uchumi.

Ofisa ushirika wilayani hapa, Malero Malero aliwasihi wanachama wa vikundi hivyo kuheshimu mikataba ya mikopo kutoka halmashauri kwa kurejesha fedha kwa wakati ili kiasi kinachopatikana kinufaishe vikundi vingine.

Chanzo: mwananchi.co.tz