Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana wang’amua fursa ufugaji kuku

KUKUU 0 Vijana wang’amua fursa ufugaji kuku

Sun, 27 Aug 2023 Chanzo: Mwananchi

Wakati tatizo la ajira kwa vijana likiendelea kuwakumba vijana nchini, baadhi ya vijana wameiona fursa kupitia ufugaji wa kuku. Baadhi ya vijana kutoka mkoani Tanga wanaotekeleza mradi wa Tanga Yetu, sasa wameanza kupata matumaini ya kujiajiri baada ya kupata mafunzo ya ufugaji kuku kibiashara kupitia kampuni ya AKM Glitters Ltd. Kampuni hiyo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga imewakusanya vijana wapatao 50 na kuwapa mafunzo ya ufugaji kuku aina ya kuroiler kibiashara kwa miezi sita na sasa wanakaribia kumaliza mafunzo hayo.

Akizungumzia mafunzo hayo jijini Dar es Dar es Salaam, Halid Masoud anasema awali hawakuwa na mwelekeo wa maisha, lakini walipounganishwa katika mradi huo, wamepata ujuzi utakaowafungulia maisha. “Tuliingia kwenye mradi huu, baada ya Halmashauri ya jiji la Tanga kutangaza kwa vijana wanaotaka kujihusisha na ufugaji wa kuku, tukajiunga. Maofisa wa maendeleo wa kata ndiyo waliotutafuta na kutuunganisha na mradi huu kupitia majukwaa yetu,” anaeleza. Amesema katika mafunzo hayo wamejifunza uatamiaji wa mayai hadi kifaranga kipatikane na jinsi ya kuvitunza katika hatua za awali. “Kutokana na mafunzo haya, tunaweza kufuatilia wafugaji tunapowapa vifaranga ili kama kuna changamoto yoyote tunawasaidia. “Kila tunapopeleka vifaranga sokoni, faida ikipatikana inakuwa ni ya kwetu, hadi sasa tuna zaidi ya Sh6 milioni katika kikundi chetu chenye watu 10 kwa miezi mitano ambayo tumekuwa kwenye mafunzo,” anasema. Kwa upande wake, Tajiri Sebe tangu alipoingia kwenye mradi huo sasa amepata ujuzi wa ufugaji kibiashara. “Tangu nilipoingia kwenye huu mradi nimefaidika kujifunza kufuga kuku, mafunzo haya yataniwezesha kufanya ujasiriamali wa kufuga kuku kienyeji,” anasema. Katika kiwanda cha kutotolesha vifaranga cha AKM Glitters Ltd kilichopo Mbezi Beach jijini hapa, hapo pia vijana hao wamepata mbinu za kuatamia, kutotolesha na kuuza vifaranga. Eneo jingine lipo Mbopo Madale (Dar es Salaam), Bagamoyo na Mkuranga (Pwani) na Sumbawanga (Rukwa).

Shamba la Mbopo Madale Akizungumza katika shamba la Mbopo Madale, Omari Mhina anayewakilisha kundi lingine la vijana wa Tanga Yetu, anasema wamejifunza vifaranga kutoka siku ya kwanza hadi siku 30 baada ya hapo tunawauza kwa wafugaji. “Tunajifunza kufuga, kutengeneza chakula cha kuku na kutotolesha vifaranga. Kuna faida tunayopata kila mwezi ambayo huwa tunagawana na sasa tuko mwezi wa sita na wa mwisho wa mafunzo yetu. “Hadi sasa tumeshaona mwanga kwenye mafunzo haya, kwani sasa tunapanga kwenda kujiajiri kwa kufanya ufugaji kibiashara,” amesema. Hata hivyo, anasema pamoja na ufadhili walioupata kwenye mafunzo hayo, bado changamoto kubwa kwao ni kupata ardhi za kufugia na mitaji ya kujenga mabanda. “Tunahitaji mtaji na mtaji wa kutosha kutuwezesha kupata ardhi na kujenga mabanda kwa ajili ya kufugia tukishatoka hapa. “Tunaiomba Serikali ituunganishe na programu nyingine zitakazotatua changamoto hizi. Tunajua mikopo ipo, lakini haituwezeshi kupata ardhi wala mabanda,” anasema. Anasema mbali na kupata mafunzo, kila awamu ya kulea vifaranga hadi kuuza wamekuwa wakipata faida ya Sh1.5 hadi 1.9 milioni wanayoiweka kwenye akiba ya kikundi. Naye Zaituni Chausa amewaondoa hofu wasichana wanaodhani kuwa ufugaji hauwezekani. “Sisi tumejifunza huu ni mwezi wa sita na tumeona kuku hawa Kuroiler F1 wana faida kubwa. Wanafugika kisasa na kienyeji. Kwa mfano sisi wanafunzi kila mwezi tunaruhusiwa kuchukua baadhi ya kuku tunawafuga,” amesema. Anaongeza, “Mpaka tulipofikia hapa vijana 50 tunataka kutokomeza ule msemo kwamba vijana wa Tanga ni wavivu, kwa sababu tuna uwezo wa kujitoa kwa hali yoyote ile,” anasema. Akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi wa AKM Glitters Ltd, Elizabeth Swai anasema, mradi huo unafadhiliwa na Botner Foundation ikishirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF). “Baada ya kupata mradi huu, tulikaa na uongozi wa Mkoa wa Tanga na wao walitupa vijana. Hatukuangalia uwezo wao wa elimu, wapo waliomaliza vyuo, wengine sekondari na wengine hawajasoma kabisa, kwa sababu sisi tunaangalia vitendo zaidi,” amesema. Anasema baada ya kuwapata vijana hao, walitengeneza vikundi vitano vyenye watu 10 kila kimoja na wamefundishwa uongozi, fedha, kujitambua na mafunzo ya vitendo ya kufuga kuku. “Kazi yao hasa ni kufuga kuku kwa wiki nne, ambapo wanajinza kutoa chanjo kwa kuku na wanajifunza kutoa mafunzo kwa wafugaji wadogo walioko Tanga kuwafundisha na kuwasimamia tangu ufugaji hadi kupeleka sokoni,” amesema. Amesema ili kutatua changamoto za mitaji, wameingia mikataba na kampuni ya Efta ili kuwapa mikopo vijana hao.

Mkutano mifumo ya chakula Sekta ya mifugo ni sehemu ya mada zitakazojadiliwa katika Mkutano wa Mifumo ya Chakula barani Afrika (AGRF) unaotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, kuanzia Septemba 5 hadi 8, 2023. Mkutano huo utakaohudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan, utakuwa pia na marais kutoka baadhi ya nchi za Afrika, mawaziri, watendaji wa Serikali, wakulima na wafugaji.

Chanzo: Mwananchi