Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana 200 kunufaika na kilimo cha kitalu nyumba

Kilimo House Vijana 200 kunufaika na kilimo cha kitalu nyumba

Tue, 12 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Vijana 200 kutoka Wilaya ya Geita watanufaika na kilimo cha kitalu nyumba (green house) kupitia mradi wa nanenane unaotekelezwa na Shirika lisilo la kiserikali la Kijani Consult lenye lengo la kuwajengea uwezo kulima kilimo kinachokabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kujikwamua kiuchumi.

Katika mradi huo unaotekelezwa kwenye kata tano wilayani humo kwa gharama ya Sh200 milioni, vijana 25 kati yao wamepewa mafunzo ya uongozi ili waweze kuhamasisha vijana wenzao kujiunga kwenye kilimo kwa kuwa na mashamba darasa yatakayokuwa ya mfano kwenye maeneo yao.

Akizungumza Septemba 11, 2023 wakati walipotembelea shughuli zinazofanywa na vijana hao Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Kijani Consult, Mandolin Kahindi amesema walengwa wamepewa mafunzo ya kujua mabadiliko ya tabia nchi ni nini, zipi athari zake na kujua njia sahihi za kukabiliana nazo.

“Tumetekeleza mradi utakaowezesha vijana kufanya kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi ili waweze kujipatia maendeleo lengo ni kuwezesha vijana kunufaika na kilimo wakati huu tunaokabiliana na mabadiliko ya tabia nchi tunataka kuona vijana wananufaika na kilimo kwa kushinda vikwazo vya kimazingira”amesema

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanufaika wa mradi huo Bahati Lubinza na Matrida Filipo wamesema kilimo cha kutumia kitalu nyumba kinawasaidia kulima wakati wote uwe wa mvua au jua bila kuwa na hofu ya mazao kuathiriwa na ukame.

“Hapa tunalima nyanya ndefu ambayo ukilima nje haihimili misukosuko kama mvua nyingi, upepo na jua kali hii inadumu muda mrefu ndani ya miezi sita hadi nane ukiwa unachuma kwa kutumia kitalu nyumba mazao yako yanakuwa hayana viatilifu tofauti na kulima nje unatumia viatilifu vingi kuua wadudu lakini pia mazao ni machache mana ni kilimo cha muda mfupi,”amesema Davitha James anayefanya kilimo hicho akata ya Ihanamilo

Ofisa ugani kata ya Nyanguku, Juma Hamad akizungumzia mradi wa kitalu nyumba amesema kilimo hicho ni suluhisho la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwakuwa kitawezesha vijana kuzalisha kwa mwaka mzima na kujiongezea kipato.

Ofisa kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Maliki Athumani amesema halmashauri hiyo imekuwa ikitumia asilimia 10 za mkopo kwa vijana kuwekeza kwenye kilimo na kila kata wametengeneza mashamba darasa ambayo vijana wanajifunza namna ya kulima kilimo bora kitakacho wanufaisha.

Naye Ofisa kilimo Halmashauri ya mji, Notkery Mwalongo amesema halmashauri hiyo imejenga vitalu nyumba sita ambavyo vinawasaidia wakulima kuzalisha mazao ya bustani ambayo yanakidhi viwango vya soko.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live