ZAIDI ya vijana 13,870 wamepata ajira katika miradi ya fedha za mapambano ya ugonjwa wa Covid-19.
Miradi hiyo inatekelezwa katika sekta za maji safi na salama, ujenzi wa hospitali 11 za wilaya pamoja na miradi ya ujenzi wa shule za ghorofa na sekta ya kilimo.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Ali Suleiman Ameir wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Chumbuni, Miraji Khamis Kwaza aliyetaka kujua miradi ya Covid-19 kwa kiasi gani imesaidia ajira kwa vijana wa Zanzibar.
Ameir alisema miradi ya fedha za Covid- 19 inatekelezwa katika sekta ya maji, afya, elimu na mafunzo ya amali, kilimo, ufugaji, asali na vijana wanaotumia dawa za kulevya.
“Kwa mfano, katika sekta ya elimu ambayo inahusisha utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa shule za ghorofa pamoja na shule za elimu mjumuisho, jumla ya ajira 7,119 zimewahusisha vijana,” alisema.
Alisema pia ajira zimepatikana katika utekelezaji wa miradi ya sekta ya elimu inayohusisha ujenzi wa shule kwa kutumia wakandarasi mbalimbali.
Kwa upande wa sekta ya afya, alisema hospitali 11 za wilaya zinatarajiwa kujengwa Unguja na Pemba ambazo zitatoa zaidi ya ajira 2,331.
Alisema ujenzi wa hospitali za wilaya unafanyika Unguja na Pemba kwa kasi kubwa na hivyo vijana wengi kupata ajira ikiwamo kazi za kusambaza vifaa vya ujenzi ikiwamo mchanga.
''Miradi ya Covid-19 inayotekelezwa na Serikali ya Zanzibar imesaidia kwa kiasi kikubwa kutoa ajira kwa makundi mbalimbali wakiwemo vijana,'' alisema.
Alisema miradi inayotekelezwa kwa fedha za Covid-19 katika sekta ya uvuvi inatarajiwa kutoa ajira kwa makundi ya vijana 4,473 wakiwemo wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo.
“Miradi ya uchumi wa buluu itawahusisha wakulima wa kilimo cha mwani kuongeza kasi ya uzalishaji pamoja na wafugaji wa samaki na majongoo ya baharini,” alisema.
Serikali ya Zanzibar imepata mgao wa fedha za kupambana na ugonjwa wa Covid-19 Sh bilioni 239 ambazo zimeidhinishwa kutumika katika sekta ambazo zimeathirika na janga hilo.