Vifaa vya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mkoa wa Mwanza vyenye thamani ya Sh233.46 milioni vimetelekezwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2021/22 vifaa hivyo ni vigae vya sakafu, ubao wa saruji na nyuzi, mabati, nondo, saruji, vigae vya ukutani, rangi ya mafuta (silk) na rangi ya nje (weather guard).
Katika taarifa yake CAG amesema ujenzi wa jengo la uwanja wa ndege wa Mwanza ulikadiriwa kugharimu Sh13.25 bilioni ambao ulipangwa kuanza Septemba 19, 2019 na kukamilika Mei 30, 2020.
“Nilibaini kuwa, Sekretarieti ya Mkoa ilipokea jumla ya Sh12.29 bilioni kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa jengo la uwanja wa ndege wa Mwanza,”imesema taarifa ya CAG, Charles Kichere.
CAG ametaja vyanzo hivyo vya fedha ni Wizara ya Fedha na Mipango iliyotoa zaidi ya Sh9.4 bilioni, Halmashauri ya Ilemela iliyotoa zaidi ya Sh1.4 bilioni na Halmashauri ya Jiji la Mwanza iliyotoa Sh1.4 bilioni.
“Zaidi ya hilo, nilibaini kuwa kufikia Disemba 2022, shughuli za ujenzi katika mradi huo zilikuwa zimesimama. Hata hivyo, vifaa vya ujenzi vilivyonunuliwa vyenye thamani ya Sh233.46 milioni vilitelekezwa katika eneo hilo kwa kipindi cha kuanzia miezi 6 hadi 24,”amesema CAG
Amesema kukosekana kwa mpango na usanifu majengo ulioidhinishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na kutoshirikishwa kwa wadau muhimu, kulisababisha marekebisho ya mara kwa mara ya miundo mbinu ya ujenzi hivyo kusababisha kusimamishwa kwa ujenzi huo tangu Juni 2022.
“Sekretarieti ya Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na TAA wanapaswa kutatua kero zinazohusu ujenzi wa kituo cha uwanja wa ndege Mwanza ili kuruhusu kukamilika kwa mradi huo na kuepuka hasara inayoweza kutokea kwa vifaa vilivyonunuliwa kupoteza ubora wake,”amesema