Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vanila; zao jipya linalotarajiwa kuinufaisha Rungwe

Ea1038ce13a2cb117f72b02e0337b679.png Vanila; zao jipya linalotarajiwa kuinufaisha Rungwe

Tue, 1 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WILAYA ya Rungwe mkoani Mbeya ni moja kati ya wilaya zilizojaaliwa kuwa na hali ya hewa rafi ki na udongo wenye uwezo wa kustawisha mazao ya aina mbalimbali.

Wakazi wa wilaya hii yenye halmashauri mbili za Rungwe na Busokelo, wanalima mazao mbalimbali yakiwemo cha chakula na biashara na kusaidia kulisha miji mikubwa ya Dar es Salaam na Dodoma.

Miongoni mwa mazao ya kibiashara yanayolimwa Rungwe ni chai na kakao inayolimwa katika eneo la Mwakaleri linalopakana na wilaya ya Kyela. Ni mara chache sana kukutana na zao lisilostawi katika wilaya ya Rungwe kwa kuwa mazao kama ndizi, viazi mviringo, viazi vitamu, magimbi, nanasi na matunda mengine yanalimwa pia kwa wingi Rungwe.

Kutokana na hali hiyo, ni nadra kusikia Rungwe imeishiwa chakula. Lakini sasa katika kukuza kipato na kuondokana na kilimo cha mazoea wilaya hii imejipanga kimkakati kuongeza mazao ya biashara.

Miongoni mwa mazao ambayo sasa yatakuwa ya kimkakati wilayani hapa ni zao la vanila linalotajwa kuwapa utajiri watu wengi duniani waliothubutu kulilima. Vanila ni kiungo ghali duniani baada ya zao la safron ambalo hulimwa sana katika nchi za Asia.

Zao hili hutumika kama kiungo katika kuongeza ladha kwenye vyakula la keki, maandazi, biskuti, barafu, uji, mtindi, juisi na soda. Ofisa habari wa Halmashauri ya wilaya ya Rungwe, Noah Kibona anasema vanilla iliyobatizwa jina la ‘dhahabu ya kijani’ inakwenda sasa kuwaneemesha wakulima wilayani hapa.

Kibona anasema hali ya hewa ya mvua nyingi na joto la wastani pamoja na udongo wenye rutuba unafanya mazao mengi kustawi bila shida wilayani Rungwe ikiwemo vanila.

Anasema uwekezaji mpya katika kilimo wilayani hapa sasa umebebwa na zao la vanila ambalo limeanza kulimwa karibu kona zote ndani ya halmashauri ya wilaya ya Rungwe na kaya nyingi zimeanza kulichangamkia kwa kuwa ni zao ambalo halihitaji eneo kubwa na linaweza kuchanganywa ndani ya mazao mengine.

Ofisa habari huyo anasema vanila inaweza kustawi vyema Rungwe kwani ni zao linalohitaji nyuzikoto kati ya 25 hadi 35 mwinuko wa mita 1,000 hadi 1,500 kutoka usawa wa bahari.

Anasema pia hustawi katika eneo linalopata mvua kati ya mililita 2500 mpaka 5000 na huhitaji takribani miezi miwili ya kiangazi ili kuruhusu maua kuchanua. Mizizi yake husambaa juu ya udongo uliosheheni mbolea ya mboji.

Vanila hutambaa kama tambazi hivyo miche yake hutiwa ardhini na kisha kuning’inizwa kwenye mti ambao hubeba shina zima la vanila. Mti unaobeba shina la vanila unapaswa uwe umeoteshwa ili kuepuka kuoza na kudumu kwa muda mrefu. Miti kama kisamvu mpira na mibono hutumika zaidi kwa kuwa huchipua mapema na hali ya hewa ya Rungwe ni rafiki kwa miti ya aina hii hiyo.

“Kiuatilifu cha mkojo wa ng’ombe kimependekezwa kuua wadudu wasumbufu ambapo mkojo huo huhifadhiwa kwenye chupa ya lita tano kwa siku 14 na kisha kuchanganywa kwenye pampu ya lita 20 tayari kwa upuliziaji,” anasema Kibona.

Anasema vanila inashauriwa kutumia samadi na mazoea mbalimbali ya mimea ili kurutubisha ardhi, kwa maana ya kilimo hai kisichotumia mbolea.

“Ukiangalia kwa hapa wilayani kwetu haya yote yanapatikana. Kwakuwa tunafuga mifugo kupata viuatilifu vinavyopendekezwa au kupata samadi ni jambo rahisi kwetu. Lakini pia maozea yapo mengi kwa kuwa tunalima pia migomba,” anasema ofisa habari huyo.

Vanila huzaa matunda yanayofanana na maharage na urefu wake huwa kati ya sentimita 10 hadi 25. Mmea huu huweza kukua na kufikia urefu wa mita 15 hadi 20. Maua yake huwa makubwa, manene na hunukia.

“Zao la vanila ni geni katika wilaya ya Rungwe hivyo hata upatikanaji wa miche au vipando vyake bado tunategemea uwezeshaji kutoka maeneo mengine. Pamoja na kwamba Kagera ndio mkoa unaozalisha kwa wingi vanila lakini inashauriwa kuagiza mbegu kutoka Uganda kwa kuwa ugonjwa wa mnyauko wa migomba umeenea mkoani Kagera,” anasema Kibona.

Anafafanua kwamba Rungwe wanahofu kuchukua mbegu Kagera kwa hofu ya kuathiri migomba yao kwa mnyauko kwa kuwa vanila hulimwa kwa kuchanganywa na migomba na mimea mingine rafiki.

Mtaalamu wa Kilimo wilayani Rungwe, Juma Mzala anasema mpaka wanaanza kuhimiza kilimo cha vanila wameshafanya utafiti na kujiridhisha juu ya soko la zao hilo. Anabainisha kuwa vanila huuzwa sana katika nchi za Ulaya na Marekani ambapo kwa sasa bei ya kilo moja hufikia shilingi 100,000 na zaidi.

Mzala anabainisha kuwa mpaka sasa wilayani hapa zaidi ya miche 61,000 imepandwa na lengo ni kuwafikia wakulima wapato 600 kwa mwaka huu ambapo inakisiwa kuwa idadi hiyo ya wakulima itaweza kuzalisha tani 222.5 zenye thamani ya sawa na zaidi ya Sh bilioni 22.

Akizungumzia mtandao wa kilimo cha vanila Rungwe, Mzala anasema mpaka sasa baadhi ya kata zilizoanza kulima zao hilo ni Kiwira, Kyimo, Bagamoyo, Ibigi, Mpuguso, Kisondela, Nkunga, Kinyala na Lupepo.

Anasema kata nyingine zinaendelea na maandalizi katika hatua mbalimbali kuelekea kulima zao hilo. Anasema mwitikio mkubwa wa wakulima zao hilo umeonekana zaidi katika kata ya Kiwira na Kyimo ambapo zaidi ya wakulima 100 tayari wamepanda vanila.

Mmoja wa wakulima katika kijiji cha Kisondela, Andrew Mwike anasema hadi sasa amefanikiwa kupanda miche 100 katika kiunga kidogo cha shamba lake huku akiahidi kuongeza zaidi idadi ya miche.

“Nilianza kilimo cha vanila kwa kupanda miche 50 lakini nikahamasika kuongeza mingine 50 na kwa sasa nina uhakika kupata mazao mengi. Nitaandaa semina niwahamasishe wenzangu makanisani na kwenye mikutano ya hadhara nao walime vanilla. Hii ni kwa kuwa nauona mwelekeo mzuri wa maisha yetu,” anasema Mwike.

Zao hili limewafurahisha wakazi wengi wilayani Rungwe kwani kutokana na uhaba wa ardhi wanaweza kulichanganya na mazao mengine kama kahawa, migomba, chai na mazao mengine ya miti.

Mchungaji Anyigulile Kasake anaiona fursa ya kilimo cha zao hili kwa kuwa anakabiliwa pia na changamoto ya uhaba wa ardhi kwenye familia yake. Familia yake inamiliki shamba lenye ukubwa wa ekari mbili tu ambazo zote alikwishapanda migomba.

Lakini sasa ndani ya ekari hizo anasema ana uwezo wa kupanda vanila pia na tayari amepanda vanilla akitarajia kuvuna zaidi ya kilo 200. Mchungaji Kasake ambaye pia ni mkazi wa Kata ya Kyimo amejikusanyia wakulima wengi wa vanila wakiwemo waumini wake ambapo kwa kushirikiana sasa wameanzisha shamba darasa ambalo linatumika kufundishia wakulima wengine.

Ofisa kilimo, Mzala anaunga mkono mshikamano huu na kushauri maofisa ugani walio karibu yao kuendelea kuwapa ushauri wa karibu ili kukiboresha kilimo cha zao hilo. Mzala anasisitiza kuwa wanunuzi wa zao hili wapo tayari kwani wamekwishafanya mazungumzo na Kampuni ya Natural Extract Industry ya mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kununua vanila yao mara msimu utakapowadia.

Halmashauri ya wilaya ya Rungwe inasema ujio wa zao hili siyo tu kwamba utaongeza kipato kwa wakulima na halmashauri kwa kuuza mazo pekee bali pia kunaongeza fursa nyingine katika Sekta ya utalii hasa utalii wa kilimo.

“Utalii wa namna hii waweza kuwa mgeni miongoni mwa wakazi wa wilaya ya Rungwe lakini kuna watu tangu wazaliwe hawajawahi kuona mmea wa chai, parachichi, kahawa na zao la vanilla,” anasema ofisa habari huyo.

Chanzo: habarileo.co.tz