Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIWANDA YATANGAZA VIPAUMBELE 10

E1924f8766afb19d1f16cfc2a2b3da91.jpeg VIWANDA YATANGAZA VIPAUMBELE 10

Sun, 23 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WIZARA ya Viwanda na Biashara imekuja na vipaumbele 10 ili sekta hizo za viwanda na biashara zichangie katika uchumi, pato la taifa na katika kuzalisha ajira nchini.

Aidha, Bunge limeiidhinishia wizara Sh 105,670,459,000. Kati ya hizo, Sh 52,582,573,000 ni za matumizi ya kawaida na Sh 53,087,886,000 ni za maendeleo.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara hiyo kwa mwaka 2021/22, Waziri wa wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo (pichani) , alisema vipaumbele hivyo ni kuendeleza na kulinda viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini pamoja na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya ngozi, nguo na mavazi.

Vingine ni kuhamasisha, kuendeleza na kulinda viwanda vya kuzalisha chuma na bidhaa za chuma na kuweka msukumo na mazingira mazuri kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vya kuunganisha vifaa vya kielekroniki na magari.

Kuhamasisha viwanda vinavyozalisha vifaa vya ujenzi, kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kutengeneza betri na umeme wa magari kwa kutumia rasilimali asili za nchi kama vile madini ya Lithium, Vanadium na Titanium na kuweka mazingira wezeshi kisera na kisheria ya kufanya biashara.

Alisema kipaumbele kingine ni kujiunga au kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika jumuiya za kiuchumi na kimasoko za kikanda kwa ajili ya kupanua fursa za kibiashara kwa bidhaa za Tanzania na kuimarisha upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali na wafanya biashara wadogo.

“Pia kuweka mazingira bora kisera, kisheria na kiutendaji kwa ajili ya kuchochea na kulinda ukuaji wa sekta binafsi kama injini na msingi wa ujenzi wa uchumi wa viwanda na shindani.”

MIRADI NA KAZI 15 Waziri Kitila alisema kwa mwaka wa fedha 2021/22, wizara imepanga kutekeleza programu, miradi na kazi 15.

Alitaja miradi na kazi hizo kuwa ni kukamilisha mapitio ya sera na sheria zinazoongoza sekta ya viwanda na biashara na kujenga mitaa ya viwanda ya kitaifa na kuhamasisha ushiriki wa mamlaka za serikali za mitaa kujenga mitaa ya viwanda katika maeneo yao kwa kushirikiana na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO).

“Hii ni pamoja na kuanza ujenzi wa Mtaa wa viwanda wa Kurasini wenye kujumuisha kongano ya viwanda vya kuchakata na kusindika mazao, viwanda vya kuunganisha vifaa vya kielekroniki, na ukanda maalumu wa biashara ya kimataifa.”

Alisema pia kusimamia utekelezaji wa miradi ya kielelezo na kimkakati, ikiwamo ya miradi ya Makaa ya Mawe wa Mchuchuma na Chuma cha Liganga, Mradi wa Magadi Soda katika Bonde la Engaruka, Mradi wa Kilimanjaro Machine Tools (KMTC), Mradi wa Viwanda katika Ukanda Maalum wa Kiuchumi wa Bagamoyo na mradi wa Ujenzi wa Mtaa wa Viwanda TAMCO – Kibaha.

Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, wizara imepanga kufanya tathimini ya kina kuhusu mafanikio na changamoto za utekelezaji wa miradi ya maeneo na ukanda maalumu wa kiuchumi (EPZ/SEZ) ili kuyaweka maeneo hayo katika muktadha wa Tanzania na dunia ya leo na kukamilisha kanzidata ya viwanda na biashara nchini.

Serikali itaendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini, kukamilisha taratibu za kuwapata wawekezaji wapya wa viwanda vilivyobinafisishwa na baadaye kurudishwa serikalini na kuimarisha mfumo wa usajili wa kampuni na leseni za biashara kupitia Wakala wa Usajili na Leseni za Biashara (BRELA).

Alisema pia kuimarisha Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Wajasiriamali Wadogo kwa kupanua wigo wa mtaji wa mfuko huo na kuratibu na kusimamia uanzishwaji wa maeneo maalumu ya kibiashara kwa lengo la kuchochea masoko kwa bidhaa za ndani na biashara ya kimataifa nchini.

Profesa Mkumbo alisema kuimarisha na kukuza matumizi ya utafiti na maendeleo, teknolojia na ubunifu katika sekta ya viwanda na biashara na kuendelea kusimamia viwango vya ubora na kubuni viwango vipya kwa ajili ya bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa Tanzania kupitia TBS na Wakala wa Vipimo (WMA).

SUKARI Waziri alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuongeza uzalishaji wa sukari kwa kupanua na kuongeza uwezo wa viwanda vikubwa vilivyopo, ikiwemo Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, pamoja na kuanzisha viwanda vikubwa vipya.

Alisema, Serikali imeelekeza taasisi ya TEMDO kufanya usanifu na kuanza kutengeneza mitambo midogo ili kuwawezesha wajasiriamali wadogo kuanza kuchakata miwa ili kupata sukari.

Alisema viwanda vyote nchini vina uwezo wa kuzalisha tani 462,863 za sukari kwa mwaka.

“Uwezo huo wa uzalishaji ni pungufu ya mahitaji ya sukari nchini ambayo ni wastani wa tani 635,000 kwa mwaka inayojumuisha tani 470,000 za matumizi ya kawaida na tani 165,000 za matumizi ya viwandani,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz