Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Sababu zilezile kutonunuliwa kwa makontena ya Makonda

Sun, 9 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Sababu ya kutouzika kwa makontena 20 ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda imetajwa kuwa ni bei kubwa inayotozwa na Mamlaka ya Mapato (TRA). Makontena hayo yanayoelezwa kuwa na viti na meza yako katika Bandari Kavu ya Dar es Salaam (DICD).

Jana baada ya makontena hayo kukosa wanunuzi kwa mara ya tatu mfululizo tangu yalipoanza kupigwa mnada Agosti 25, wateja walieleza kuwa bei ndiyo kikwazo.

Kabla ya jana, mnada wa kwanza wa makontena hayo ulifanyika Agosti 25, wa pili Septemba Mosi na yote yamekosa wanunuzi.

Wakizungumza baada ya mnada kumalizika bila kununuliwa jana, wateja waliojitokeza walisema bei iliyowekwa na TRA ni kubwa tofauti na wao wanavyotaka.

Walisema wao wakiwa ni wafanyabiashara wanajua thamani halisi ya samani zilizomo ndani na endapo wazitanunua kwa bei inayotajwa ya Sh60 milioni watapata hasara katika kuziuza.

Mmoja wa wanunuzi, Jimmy Cosmas alisema kununua kontena lenye bidhaa za aina hiyo haizidi Sh30 milioni, lakini TRA wanauza kwa Sh60 milioni.

“Wanunuzi wapo, wakishusha bei yatanunulika mimi nafanya biashara najua kwa bei hiyo waliyopewa (madalali) wasitegemee kuuza,” alisema Cosmas.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya udalali ya Yono, Scolastica Kevela alisema wao wanatekeleza jukumu walilokabidhiwa na TRA na kwamba, wateja wao wamefika bei waliyofikia.

Alisema wanasubiri maelekezo mengine kutoka mamlaka hiyo ili kujua nini cha kufanya. “Kama mnavyoona samani hazijanunulika wateja wamejitokeza ila bei wanayoishia ni (Sh) 2O hadi 3O milioni, tunasubiri maelekezo mengine ya TRA,” alisema Scolastica.

Katika mnada wa pili wa Septemba Mosi, mmoja wa wateja, Ibrahim Jongo alisema makontena hayo hawakuyanunua kwa sababu bei ni kubwa na ujazo wa bidhaa ni mdogo. “Hata kama ni wewe uambiwe kontena lile ni Sh10 milioni au Sh20 milioni utanunua? Kwa sababu walivyopakia ni kama wamelundika,” alisema. Mei mwaka huu, TRA ilichapishwa kwenye gazeti la la Daily News ikiwataka wamiliki wa mali zilizokaa bandarini kwa zaidi ya siku 90 kujitokeza kuzilipia. Orodha ya wamiliki hao ilionyesha jina la mtu aitwaye Paul Makonda aliyekuwa na makontena 20.

Kadhalika tangazo hilo lilitishia kuzipiga mnada mali hizo iwapo wamiliki hawatajitokeza ndani ya kipindi hicho.

Hata hivyo, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda aliyakana makontena hayo akisema si yake.

“Sidhani kama nahusika na jambo lolote lile na sijui chochote. Hilo unalolisema hata mimi nimesoma kwenye magazeti kama ulivyosoma wewe, nafikiri zilikuwa ni habari za jana na leo nimesoma nyingine,” alisema Makonda wakati huo. Makonda alisema Serikali hufanya kazi zake kwa kutumia maandishi na yeye hana nakala yoyote inayohusiana na mzigo huo.

Baadaye, Mei 20 ilisambaa barua ya TRA ikieleza kuwepo kwa ombi la msamaha wa kodi ya mali hizo kutoka kwa Makonda kwenda kwa waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.

Agosti 31, siku moja kabla ya Septemba Mosi ulipofanyika mnada wa pili, Rais John Magufuli alizungumza na madiwani, viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita na kuwataka viongozi kujenga mazingira ya kuwatumikia wananchi bila kujali nafasi zao.

Alitolea mfano sakata la makontena ya Makonda baada ya kushindwa kuyalipia kodi bandarini.

“Umesikia hili sakata la Dar es Salaam, eti mkuu wa mkoa ameleta makontena, ameambiwa alipe kodi, kwa nini asilipe kodi?” alihoji Rais.

Bila ya kumtaja jina, Rais Magufuli alisema sheria za nchi zinasema ni mtu mmoja pekee katika nchi mwenye dhamana ya kupokea msaada kwa niaba ya wananchi kwa mujibu wa sheria ya fedha, sheria ya madeni, sheria ya dhamana na ya misaada.

Aliitaja sheria hiyo ni namba 30 ya 1974, kifungu cha 3, 6, 13 na cha 15 kuwa ndivyo vinampa mtu huyo dhamana ya kupokea misaada. “Hakuna mtu mwingine. Sasa ukichukua makontena kule, umezungumza na watu wengine labda na wafanyabiashara unasema ni makontena yako, halafu ukasema tena labda ni ya walimu, wala hata shule hazitajwi, maana yake nini?”

“Maana yake si unataka utumie walimu ulete haya makontena, utapeleka shule mbili au tatu ndizo zitapewa, mengine unakwenda kuyauza unapeleka kwenye shoping mall (maduka makubwa). Lakini walimu walikuambia wanahitaji makochi, sofa.”

Chanzo: mwananchi.co.tz