Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Mnada wa nne makontena ya Makonda watoka kapa

17588 Pic+mnada TanzaniaWeb

Mon, 17 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kwa mara ya nne makontena 20 ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda yalishindwa kuuzika bandarini jana kwa kukosa wanunuzi.

Watu wachache waliojitokeza kwenye mnada huo walijaribu kutaja bei kila kontena lilipokuwa likitajwa, lakini hakuna hata mmoja aliyefanikiwa kununua moja kati ya makontena hayo.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mnada huo, mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya udalali ya Yono, Scolastica Kevela alisema hakuna mteja aliyepatikana.

Scolastica ambaye kampuni yake imepewa kazi ya kupiga mnada makontena hayo kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), alisema bei zinazofikiwa na wateja hazifikii malengo waliyowekewa.

“Ni kweli wateja wanakuja na bei lakini bado hazijafikia zile ambazo TRA wametuwekea kama kodi yao. Tunaomba watu wajitokeze kununua mali hizi ili Serikali ipate kodi,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema wao kama madalali wataendelea kufanya utafiti kupata wateja.

Ufafanuzi wa TRA

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Walipakodi TRA, Richard Kayombo alieleza kuwa wataendelea kuyapiga mnada makontena hayo na pale itakapoona yameshindwa kununulika watafuata utaratibu mwingine ambao umeelekezwa kisheria.

“Tukiona yameshindakana kabisa kununuliwa tutafuata maelekezo ya sheria, huko tutaaangalia tugawe mali zilizomo au utaratibu gani mwingine ufanyike,” alisema.

Makontena hayo yenye samani kama viti, meza na mbao za kuandikia yanadaiwa kodi inayokadiriwa kuwa Sh1.2 bilioni.

Minada iliyofanyika

Kwa mara ya kwanza makontena hayo yalipigwa mnada Agosti 25, lakini yalikosa wanunuzi kutokana na watu wengi kushindwa kufikia bei iliyotakiwa, baadhi yao wakitaja Sh10 milioni kwa kontena badala ya Sh60 milioni inayotakiwa.

Baada ya makontena hayo kutouzika, Agosti 26, Makonda alitoa onyo akiwa mkoani Kagera kuwa mtu atakayeyanunua atalaaniwa yeye (mnunuzi) na uzao wake.

Agosti 27, waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango alikwenda bandarini kuyakagua na kuwataka viongozi wenzake serikalini kutathmini kauli zao na akawaomba watu wanaotaka kununua samani hizo wasiogope.

Akizungumza na madiwani, viongozi na watumishi wa Halmshauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita Agosti 30, Rais John Magufuli alipigilia msumari sakata hilo akiwataka viongozi kuwatumikia wananchi bila kujali wapo kwenye nafasi gani.

“Umesikia hili sakata la Dar es Salaam, eti mkuu wa mkoa ameleta makontena, ameambiwa alipe kodi, kwa nini asilipe kodi?” alihoji Rais Magufuli. Alisema sheria za nchi zinasema ni mtu mmoja katika nchi mwenye dhamana ya kutolipa kodi kwa mujibu wa sheria ya fedha, sheria ya madeni, sheria ya dhamana na ya misaada.

“Sasa ukichukua makontena kule umezungumza na watu wengine labda na wafanyabiashara, unasema ni makontena yako halafu ukasema tena labda ni ya walimu, wala hata shule hazitajwi maana yake nini,” alisema Rais.

“Maana yake si unataka utumie walimu ulete haya makontena, utapeleka shule mbili au tatu ndizo zitapewa, mengine unakwenda kuyauza unapeleka kwenye shoping mall (maduka makubwa). Lakini walimu walikuambia wanahitaji makochi, sofa.”

Septemba Mosi ulifanyika mnada mwingine, lakini kwa mara nyingine makontena hayo hayakuuzika kutokana na wateja kushindwa kufikia bei iliyotajwa.

Kadhalika Septemba 8 ulifanyika mnada mwingine.

Makonda ashtukia mikopo

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda aliwataka wakazi wa Dar es Salaam kuorodhesha mikopo inayohusisha hati za nyumba wasiyoitambua kwenye ofisi za wakuu wa wilaya kuanzia kesho.

Makonda alisema lengo la kufanya hivyo ni kutafuta ufumbuzi wa wananchi wasio na uelewa wa masuala ya benki ambao wamekuwa wakitapeliwa hati za nyumba na kisha nyumba zao kuuzwa.

Alisema wamebaini aina ya utapeli unaoshika kasi hivi sasa wa kutumia hati za nyumba zilizowekwa kama dhamana ya kukopea benki na watu mbalimbali.

Alifafanua kuwa anayewekewa dhamana anakwenda kukopa fedha nyingi benki kwa kutumia hati ya nyumba ya mtu, kisha anatelekeza mkopo na watu wa benki wanapiga mnada nyumba husika wakati mwenyewe hakukopa kwao.

Alisema baada ya kuorodhesha mikopo hiyo wiki inayofuata watakutana na benki zote 56 zilizopo jijini Dar es Salaam kujadili namna ya kutatua changamoto hiyo.

“Kwa muktadha huu aliyechukua mkopo benki hana shida anaendelea na shughuli zake, tatizo linakuja kwa mwenye hati ambaye hajui lolote, nyumba yake inapigwa mnada,” alisema Makonda.

Alisema kwa sasa kuna kesi zaidi ya 500 zinazohusu utapeli wa aina hiyo zikihusisha hati za nyumba na viwanja ambazo zinatosha kuanzia, lakini wameona wawape fursa wananchi kuorodhesha migogoro kwa watu ambao hawakupata nafasi ya kufanya hivyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz