Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Mfanyabiashara aliyetajwa na Majaliwa adai hasara Sh800mil

Mon, 10 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ramadhani Ntunzwe aliyetajwa na Rais John Magufuli kuwa miongoni mwa wafanyabiashara waliowahi kusumbuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ameibuka na kusimulia mkasa mzima huku akidai kupata hasara ya Sh800 milioni.

Rais Magufuli alitoa maagizo kwa Takukuru kuwakamata na kuwafikisha mahakamani maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waliohusika kumsumbua mfanyabiashara huyo kwa kushikilia mali zake kwa miaka mitatu bila sababu za msingi.

Baada ya mkutano huo wa juzi, jana kulifanyika mabadiliko ya baadhi ya viongozi ikiwamo Rais kumuondoa kamishina mkuu wa TRA, Charles Kichere na kumteua Edwin Mhede.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ndiye aliyelianzisha sakata hilo alipokuwa akizungumza katika mkutano wa wafanyabiashara ulioitishwa na Rais John Magufuli, Ikulu ya Dar es Salaam juzi.

Mkurugenzi wa Elimu na Uhusiano wa TRA, Richard Kayombo alipoulizwa kwa simu kuhusu suala hilo alisema hawezi kuzungumzia kwa kuwa maelekezo yameshatolewa na tayari hatua zimeshaanza kuchukuliwa.

“Maelekezo ya kiutawala yameshatolewa na kama ulivyoona hatua zimeanza kuchukuliwa,” alisema Kayombo.

Pia Soma

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu jana, mfanyabiashara huyo mwenye duka katika mtaa wa Congo, Kariakoo ameelezea mkasa mzima ulivyoanza Oktoba 2016 alipokuwa akisafirisha mzigo wake kutoka Afrika Kusini kupitia mpaka wa Tunduma.

Alisema mzigo huo ambao ni mabegi, nywele za bandia na kamera za CCTV na kodi zote kwa ujumla zilimgharimu Sh50 milioni.

“Baada ya kulipa kodi zote katika mpaka wa Tunduma, nikakabidhiwa nyaraka zote nikaruhusiwa kuondoka, nilipita katika ‘check points’ zote nikakaguliwa na kupita bila shida.

“Sasa nilipofika hapo Mbezi kwa Msuguri (Dar es Salaam), lile gari semi trailer lililokuwa limebeba mzigo wangu lilipata hitilafu. Ikabidi dereva aweke gari pembeni,” anasimulia.

Alisema aliamua kwenda Kariakoo kuwachukua wafanyakazi wake na kukodisha magari mawili (Fuso na Suzuki Carry) na kwenda nayo Mbezi kuhamisha mizigo na hapo ndipo mikasa ilipoanzia.

“Hapo ilikuwa imeshafika saa 5:30 usiku. Wakati tunaendelea kufaulisha mzigo ikatokea gari aina ya Land Cruiser ikiwa na askari polisi waliokuwa patrol. Wakauliza mzigo wa nani nikawaambia wangu. Nikawapa nyaraka wakaangalia, wakajiridhisha wakasema endeleeni maana mzigo ni halali,” alisema.

“Baada ya nusu saa likaja gari jingine likiwa na askari polisi watatu, wakashuka nao pia wakauliza mzigo ni wa nani?

“Nikawaambia wangu nikawaeleza ulipotoka. Mmoja wa askari aliyejitambulisha kwa jina (anamtaja), akawaambia mnahangaika na nyaraka za nini? Yeye tu atupe mzigo wa kufa mtu tuondoke. Kwanza amesema amebeba mabegi na nywele, si kweli amebeba dawa za kulevya,” alisimulia akimnukuu mmoja wa polisi hao.

Alisema baada ya kuwakatalia katakata kuwapa rushwa wakasema kwa sababu anajifanya mjanja, wanampigia mtu wa TRA ili amkomeshe.

Baada ya mabishano hayo anasema aliamua kumpigia simu kamishna wa Polisi (aliyemtaja kwa jina) na kumueleza tukio hilo, naye akataka aongee nao kwa simu, ndipo wakamwacha.

Alisema baada ya kumaliza kufaulisha mzigo walianza kuondoka eneo hilo. Lakini walipofika Kimara Mwisho kumbe yule ofisa wa TRA aliyepigiwa simu ndiyo alikuwa amefika akiwa na askari wenye bunduki.

“Yule ofisa wa TRA (jina tunalo) alijitambulisha na kuomba nyaraka za mzigo, akaziangalia akasema mimi nafanya kazi TRA, magumashi yote nayajua. Kama unataka yaishe tupe Sh2 milioni. Nilimwambia wale askari waliompigia walitaka niwape rushwa nimekataa,” alieleza.

Hata hivyo, alisema yule ofisa wa TRA akiwa na askari wale waliendelea kushikilia msimamo wao na kumtaka ashushe mzigo chini. Baada ya malumbano ya dakika kadhaa, aliwaambia waende Kariakoo kwenye duka lake akawapatie hiyo Sh2 milioni.

Alisema walipofika Kariakoo mtaa wa Congo lilipo duka lake, alimwomba ofisa wa TRA kitambulisho chake ili ajiridhishe na kweli yule ofisa alimpa na alipokipokea aliingia nacho nyumbani kwake na kukipiga picha kisha akatoka na kumrudishia.

Kisha akamwambia hatatoa hela yoyote na ndipo malumbano yakaanza upya kiasi cha kujaza watu licha ya kuwa usiku wa manane.

“Baada ya kuona watu wengi waliamua kupiga simu kituo cha polisi Msimbazi, ghafla zikaja gari mbili za polisi zikiwa na askari zaidi ya 15 wakiwa na bunduki wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD).”

Alisema yule OCD aliwaambia waende kituoni na yale magari na huko alimhoji ofisa wa TRA kabla ya kuwahoji pia yeye na wafanyakazi wake na baada ya majadiliano ya muda mrefu usiku ule, OCD hakuona kosa, akamuachia huru.

Lakini ofisa wa TRA alimwomba OCD ampe ulinzi ayapeleke magari yale kwenye yard yao.

Baada ya siku hiyo kupita, anasema alianza kuufuatilia mzigo wake TRA ambako alianza kuzungushwa tangu Oktoba 2016 hadi Machi 2019.

Alisema wakati akiendelea kuzungushwa kupewa mzigo wake, mwaka 2018 walifika maofisa wa TRA na baada ya kujitambulisha walidai kuwa hatoi risiti za EFD.

Alipowauliza ushahidi, mmoja wao alitoa kidani akidai alikinunua kwenye duka hilo.

“Nilimkatalia kwa kuwa siuzi urembo, lakini waling’ang’ania, kumbe walikuwa wamekuja na kampuni ya udalali, na ndipo maofisa wake walipofunga milango ya duka langu.

“Wakati wakiendelea kufunga duka niliwaomba wasifunge mlango mmoja kwa kuwa ndiyo ninaoutumia kuingilia nyumbani, lakini walikataa na kuingia uani walipokuta wanawake wakiandaa futari maana ulikuwa mwezi wa Ramadhan. Walimwaga vyakula vyote na kuzima moto kwa maji.”

Alisema baada ya kumfungia duka lake walimweka mahabusu katika Kituo cha Polisi Msimbazi kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa moja jioni alipopewa dhamana.

“Baada ya miezi sita ya kufunga duka langu wakaja kufungua makufuli yao tukakuta mali yote imeibwa. Nilipata hasara ya Sh821 milioni hivi tunavyoongea.

“Ilisababisha mke wangu siku hiyo kuchanganyikiwa na alilazwa Muhimbili. Dada yangu aliyekuwa akisimamia duka hili alipata mshituko mpaka alikuja kufariki tukamzika. Nimeshindwa kusomesha watoto, nimeishi kwa mazingira magumu,” alisema.

Hata hivyo alisema bado mali zake ziliendelea kushikiliwa na TRA, licha ya kuwaeleza makamishna wa mamlaka hiyo wakiwemo makamisha wakuu wa TRA bila mafanikio.

“Machi 1, 2019 Waziri Mkuu alikuwa na kikao na wafanyabiashara pale Anatouglou. Bahati nzuri nilikuta mkutano haujaanza, baadaye nilipata nafasi nilipotoa hii kero kwa Waziri Mkuu, ndipo ikatolewa amri na Waziri Mkuu mzigo wangu urudishwe kwangu,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz